Serikali yapewa ushauri utekelezaji miradi mikubwa

Muktasari:

Profesa Ninatubu Lema ametaka wahandisi wazawa kupewa fursa zaidi

Dar es Salaam. Meneja mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro, Young-Hak Choi ameishauri Serikali kutengeneza sheria maalumu itakayosimamia miradi mikubwa.
Amesema sheria zilizopo zinawataka makandarasi kulipa tozo ya mitambo inayoingizwa nchini, hivyo kuwapo uwezekano wa kuchelewesha kukamilika miradi.
Choi amesema hayo leo Julai 17, 2018  jijini Dar es Salaam wakati wa ziara ya wajumbe wa Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB) katika mradi wa SGR.
Amesema reli ya kisasa ni muhimu kwa Watanzania hivyo ni vyema sheria zinazokwamisha mradi zikaondolewa.
Mwenyekiti wa ERB, Profesa Ninatubu Lema amewataka makandarasi wa reli hiyo kutumia wahandisi wazawa.
Amesema kazi zinazoweza kufanywa na Watanzania wapewe wafanye ili nao wanufaike na mradi wa SGR.
Profesa Lema amesema hawajaridhishwa na ushiriki wa wahandisi wazawa kwenye mradi huo, akitaka wengi zaidi watumike.
Ameipongeza kampuni ya Yapi Merkezi inayojenga reli hiyo kwa hatua iliyofikiwa.