Serikali yaahidi kutoa maelezo kuhusu zuio la kuuza mazao nje

Muktasari:

Hatua hiyo imekuja baada ya wabunge kutoridhika na majibu ya Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Uvuvi, William Ole Nasha ambapo Mbunge wa Geita Mjini(CCM), Joseph Musukuma aliyetaka kujua Serikali imejipangaje kuwasaidia wakulima ambao wamevuna na kushindwa kuuza mazao yao kutokana na kukosa soko huku ikizuia wasiuze nje.

Dodoma. Wakati wakulima wakilia kukosa soko la mazao licha ya kupata mavuno mengi Serikali inatarajia kutoa maelezo ya kina ya nini kifanyike ili kuweza kunusuru hali hiyo.

Hivi karibu Serikali kupitia Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi ilipiga marufuku wakulima kuuza mazao yao nje ya nchi jambo lililosababisha soko la mazao hayo kuyumba huku bidhaa kama nyanya zikiharibika bila kupata wanunuzi.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu- Sera, Bunge, Ajira, Kazi, Vijana na Walemavu, Jenista Mhagama akizungumza kwa niaba ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema bungeni kuwa Serikali itatoa maelezo ya nini kifanyike kabala mwisho wa wiki.

Waziri Mhagama amefikia hatua hiyo baada ya wabunge wanne kutoridhishwa na majibu yaliyotolewa na Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, William Ole Nasha ambaye alitakiwa na mbunge wa Geita vijijini (CCM) Joseph Msukuma kueleza ni jinsi gani Serikali imejipanga kuwa saidia wakulima ambao kwa sasa wamepata mavuno mazuri lakini hawana pa kuyapeleka.

Naibu Waziri Ole Nasha amesema Serikali imeliona hilo na itaweka mkakati maalumu wa kuwasaidia wakulima hao ili kuhakikisha wananufaika na mazao yao.

Kufuatia jibu hilo, Mwenyekiti aliyekuwa akiongoza Bunge, Andrew Chenge amesema kitendo cha kuwanyima wakulima uhuru wa mazao yao si sahihi na kuhoji kwa nini wafanyakazi hawapangiwi namna ya kutumia fedha zao za mshahara.

Mara baada ya kipindi cha maswali na majibu kuisha zaidi ya wabunge 10 walisimama wakiomba mwongozo lakini Chenge aliwatambua wanne na kuwapatia nafasi.

Wabunge hao ni Ali Keissy (Nkasi Kaskazini), Oscar Mkasa (Biharamulo Magharibi) Joseph Msukuma (Geita vijijini) na Ignas Malocha Kwera wote kutoka CCM.

Akitumia kifungu cha kanuni namba 46 (1) Keisy, amehoji kwa nini Serikali inawaadhibu wakulima na kuwaacha wafanyakazi waendelee kutumia mshahara wao kwa uhuru.

Keissy amepigiwa makofi na wabunge wote bila kujali itikadi zao.

Baada ya Keissy, Malocha akitumia kifungu hicho hicho amesema hakuridhika na majibu ya waziri huyo na kuomba Serikali itoe taarifa ya chakula ili wabunge waweze kujadili.

Mkasa ametumia vifungu vya 68 (7) na 46 (1) na kuhoji kwa nini waajiri wanachelewesha malipo ya pensheni kwa waajiriwa na kutaka majibu yanayokidhi haja.

Msukuma amesema alipouliza swali la nyongeza waziri hakumuelewa na kumpa majibu yasiyokidhi na akaomba waziri huyo kutoa majibu yatakayomridhisha.

Kufuatia mjadala huo, Chenge ametoa mwongozo akisema Serikali imesikia kilio chake na anaamini waziri mkuu au mawaziri wake watalitolea ufafanuzi suala hilo.

Baada ya kuona hoja hiyo inapamba moto, Waziri Mhagama amesimama na kusema kuwa kwa niaba ya waziri mkuu, Serikali itawasilisha maelezo ya kina kuhusu suala hilo na hivyo wabunge wasiwe na wasiwasi.

Hata hivyo, Chenge alimbana zaidi Mhagama na kumtaka atamke ni siku gani hasa maelezo hayo yataletwa bungeni, na waziri huyo akaahidi kabla ya wiki hii kumalizika.