‘Hakuna sheria ya posho kwa viongozi wa mitaa’

Muktasari:

Serikali imetoa kauli hiyo bungeni leo na kufafanua kuwa jambo hili liliwekewa utaratibu mwaka 2003


Dodoma. Serikali haijaweka mpango wa kuwalipa posho viongozi wa vitongoji, mitaa na kijiji. Bunge limeelezwa leo.

Naibu Waziri wa nchi ofisi ya Rais Tamisemi, Joseph Kakunda amesema hakuna sheria iliyowekwa kwa ajili kuwalipa.

Katika swali la msingi mbunge wa Magu, Boniventure Kiswaga (CCM) alitaka kujua ni lini serikali itawalipa mishahara wenyeviti wa vitongoji, mitaa na vijiji kwa kuwa Serikali inaanzia ngazi ya chini

Mbunge amepinga kauli kuwa wanaochaguliwa wanapaswa kuwa na kipato akahoji mbona wabunge wanatakiwa kuwa na kipato lakini wanalipwa mishahara.

Kakunda amesema miongoni mwa sifa zinazomwezesha Mtanzania kuchaguliwa katika ngazi hizo ni kuwa na shughuli halali ya kumuingizia kipato.

Hata hivyo amesema Serikali ilishatoa utaratibu kutoka mwaka 2003 kwamba waendelee kulipwa posho kupitia mapato ya ndani.