Ripoti kamati ya Nape kutua kwa Magufuli

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape  Nnauye (katikati) akipokea ripoti kutoka kwa Mwenyekiti wa kamati iliyokuwa ikichunguza kuhusu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kuvamia Kituo cha Television cha Clouds, Dk Hassan Abass, jijini Dar es Salaam jana. Kulia ni Katibu wa kamati hiyo, Deodatus Balile. Picha na Anthony Siame

Muktasari:

Wakati ripoti hiyo ikiwekwa hadharani, Jukwaa la Wahariri (TEF) limelaani kitendo cha mkuu huyo wa mkoa na kumtangaza kuwa adui namba moja wa uhuru wa habari nchini.

Dar es Salaam. Waziri wa Habari, Nape Nnauye amesema ripoti ya matokeo ya uchunguzi wa kitendo cha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kuingia studio za Clouds Media akiwa na askari wenye silaha za moto, ataikabidhi kwa mamlaka za juu kwa ajili ya hatua stahiki.

Wakati ripoti hiyo ikiwekwa hadharani, Jukwaa la Wahariri (TEF) limelaani kitendo cha mkuu huyo wa mkoa na kumtangaza kuwa adui namba moja wa uhuru wa habari nchini.

Kamati ya Nape

Nape alisema hayo jana kwenye ukumbi wa Idara ya Habari jijini Dar es Salaam baada ya kukabidhiwa ripoti hiyo na Dk Hassan Abbas aliyeongoza kamati ya watu watano aliyoiunda Nape kuchunguza tukio hilo lililotokea Ijumaa usiku.

“Niseme tu kwamba nimeipokea ripoti na kama nilivyosema kazi hii si rahisi sana ina gharama kubwa. Gharama ya kusimamia haki, kusimamia ukweli,” alisema Nape.

Alisema anajua kuwa ripoti hiyo si ndogo kwa kuwa ina vielelezo vingi, ikiwa ni pamoja na sauti na picha za video za watu waliotoa ushahidi na picha za CCTV zilizochukuliwa ofisi za Clouds Media.

“Sasa mimi juu yangu kuna Waziri Mkuu, kuna Makamu wa Rais na kuna Rais mwenyewe na ndio wakubwa zangu. Na hawa ndio mamlaka yangu ya juu baada yangu. Kwa hiyo, nitakachofanya ni kukabidhi hizi taarifa kwao,” alisema Nape.

Pamoja na kusema hayo, mamlaka ya kuteua na kutengua uteuzi wa wakuu wa mikoa na wilaya ni ya Rais, ambaye mapema wiki hii alisema hawezi kufanya uamuzi kwa shinikizo la mitandao ya kijamii na kumtaka Makonda aendelee “kuchapa kazi”.

Nape pia alikuwa na ushauri kwa wanasiasa wenzake. “Nikiri kwamba sisi ni binadamu. Tunaweza kuwa na madhaifu (udhaifu) ya hapa na pale. Jambo la msingi yanapotokea madhaifu haya ni vizuri kukubali kuwa kuna tatizo,” alisema Waziri Nape.

Habari zaidi soma Gazeti la Mwananchi