Pacha Maria na Consolata kuhamishiwa JKCI kwa matibabu

Muktasari:

Dk Mwakalebela amesema wanaendelea vizuri ila wanahitaji uchunguzi zaidi.

Iringa. Pacha walioungana, Maria na Consolata wanatarajia kuhamishiwa jijini Dar es Salaam kwa matibabu katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI).

Kaimu mganga mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Iringa wanakopatiwa matibabu, Dk Alfred Mwakalebela amesema pacha hao waliolazwa hospitalini hapo Desemba 28,2017 watapelekwa JKCI kwa matibabu zaidi.

Amesema tatizo la moyo linalowakabili linahitaji uchunguzi na matibabu zaidi katika taasisi hiyo.

“Hali zao zinaendelea vizuri lakini tumeona wanahitaji uchunguzi na matibabu zaidi ndiyo sababu tumeamua kuwapa rufaa,” amesema.

Dk Mwakalebela amesema leo Jumanne Januari 2,2018 kuwa uamuzi huo umelenga kuwawezesha pacha hao wanaosoma Chuo Kikuu Katoliki cha Ruaha (Rucu) cha mjini Iringa kufanyiwa uchunguzi na matibabu zaidi.