Odinga ataka marekebisho ya Katiba

Muktasari:

  • Raila amewasilisha ujumbe huo katika kikao cha Baraza Kuu la ODM ikiwa ni kati ya makubaliano yake na Rais Kenyatta

Nairobi ,Kenya. Kiongozi wa upinzani Raila Odinga amesema inabidi Katiba ifanyiwe marekebisho ili kufanikisha utelekezaji ajenda tisa ambazo yeye na Rais Uhuru Kenyatta walikubaliana Machi 9, 2018.

Amesema miongoni mwa mambo ambayo waliwekeana sahihi yeye na Rais Kenyatta ni pamoja na urekebishwaji wa Katiba ya nchi hiyo.

Odinga amesema kabla ya hapo chama hicho kitaandaa mikutano kadhaa ya hadhara kote nchini kuwaeleza na kiongozi huyo.

‘’Kushughulikiwa kwa baadhi ya masuala yaliyoko kwenye muafaka huo kutahitaji mabadiliko katika sheria zetu na hata mabadiliko katika Katiba," amesema Odinga.

Odinga amesema hayo alipokuwa akiongoza mkutano wa Baraza Kuu (NEC) la ODM katika Hoteli ya Elementaita Lodge, Gilgil.

"Wakati hayo yakijiri tunatakiwa tuwe jasiri na kulichukulia suala hilo kama wajibu wetu kwa taifa," amesema.

Huenda kauli yake ikaendelea kupandisha joto la kisiasa nchini kwani Naibu Rais William Ruto na wenzake  wanapinga wazo la Katiba kufanyiwa marekebisho kabla ya uchaguzi mkuu wa 2022 kupitia kura ya maoni.

Odinga anataka marekebisho hayo yafungamane na yaliyomo kwenye rasimu ya katiba ya Bomas iliyotayarishwa mwaka 2005.

Kwa mujibu wa Odinga, mfumo wa sasa unalimbikiza madaraka zaidi katika ofisi ya Rais, hali inayozidisha ushindani mkubwa kwa wadhifa huo.

Odinga anasema kuwa mamlaka ya ofisi tekelezi hutekelezwa na mawaziri wanaoteuliwa kutoka kwa chama chenye wabunge wengi katika Bunge la Kitaifa.

Hata hivyo, kambi ya Ruto inapinga huku ikisema marekebisho ya Katiba yatalirejesha taifa katika kipindi cha kampeni, hali ambayo itaathiri ajenda ya serikali ya Jubilee ya kutelekeza maendeleo.

"Bila mabadiliko yaliyoangaziwa katika mwafaka wa uchaguzi wa 2022 kutatokea kukanganya na ghasia. Tunajaribu kuzuia mambo kama hayo," amesema  Odinga.

Ajenda tisa ambazo ziliangaziwa katika mwafaka huo ni; kukomeshwa kwa ukabila, kurejeshwa kwa maadili ya kitaifa, uongozi jumuishi, usalama kwa Wakenya, kukomeshwa kwa ufisadi na kuhakikisha kuwa kuna maendeleo shirikishi.