Nondo awagonganisha Polisi Dar, Iringa

Mwangalizi wa Haki za Binadamu wa Mtandao wa Wanafunzi Tanzania (TSNP), Alphonce Lusako (wa pili kushoto) akizungumza na wanahabari baada ya kuhojiwa katika ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Dar es Salaam jana kuhusu tukio la kupotea kwa mwenyekiti wa mtandao huo, Abdul Nondo. Kulia ni ofisa habari wa mtandao huo, Hellen Sisya. Picha na Ericky Boniphace.
Muktasari:
Nondo, ambaye ni mwanafunzi wa mwaka wa tatu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), alidaiwa kutoweka usiku wa kuamkia Machi 6 na kupatikana usiku wa Machi 7 huko Mafinga, Iringa na kujisalimisha polisi.
Dar es Salaam. Unaweza kusema madai ya kutoweka kwa Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi Tanzania (TSNP), Abdul Nondo kumeligonganisha Jeshi la Polisi katika mikoa ya Dar es Salaam na Iringa kutokana na kutoa taarifa zinazokinzana kuhusu tukio hilo.
Nondo, ambaye ni mwanafunzi wa mwaka wa tatu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), alidaiwa kutoweka usiku wa kuamkia Machi 6 na kupatikana usiku wa Machi 7 huko Mafinga, Iringa na kujisalimisha polisi.
Machi 8, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Juma Bwire aliwaeleza waandishi wa habari kwamba walifungua jalada la uchunguzi ili kubaini iwapo Nondo alitekwa au alitoa taarifa za uongo kwa lengo la kuhamasisha wanafunzi kuvuruga amani na akabainisha kuwa mwanafunzi huyo alijisalimisha Polisi Mafinga, akidai ametelekezwa na waliomteka.
Lakini wakati Bwire akisema Nondo alijisalimisha polisi na kudai alitekwa na watu ambao walimtelekeza, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa alisema mwanafunzi huyo alionekana Mafinga akiendelea na shughuli zake na wala hakuripoti tukio la kutekwa kituo chochote cha polisi na kwamba ndio sababu ya kuendelea kumshikilia.
Wakati bado Nondo akiwa Iringa, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda alilitaka jeshi la polisi kumrejesha mkoani kwake litakapomaliza uchunguzi ili ufanyike mwingine kubaini iwapo alijiteka au la.
Machi 13, Kamanda Mambosasa alisema kwa kushirikiana na Polisi Mkoa wa Iringa, walifanya uchunguzi na kubaini kuwa mwanafunzi huyo hakutekwa, bali alijiteka mwenyewe ili kutafuta umaarufu wa kisiasa na kuzua tafrani kwa jamii.
Wengine wahojiwa kwa DCI
Jana, viongozi wanne wa mtandao huo wa wanafunzi, walihojiwa katika ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI). Waliohojiwa ni mwangalizi wa haki za binadamu, Alphonce Lusako; katibu wa mtandao huo, Malekela Brigthon; ofisa habari, Hellen Sisya na mkurugenzi wa idara ya sheria, Paul Kisabo.
Wakili wa wanafunzi hao, Reginald Martine alisema waliitwa kuhojiwa ili kutoa ushahidi kuhusu tukio la kutekwa kwa Nondo. Alisema walishauriana na mmoja wa makamishna wa polisi kuwa yeye asiwepo na viongozi hao wakati wanatoa ushahidi wao.
“Mimi Nondo ndio alinitumia meseji ya mwisho kuwa alikuwa katika sehemu si salama. Sasa tumeitwa polisi na kuulizwa kuhusu meseji yake ya mwisho, kupotea kwake, siku ambayo mtandao wetu ulizungumza na wanahabari juu ya kupotea kwa Nondo” alisema Kisabo.
Hata hivyo, viongozi hao walilalamikia polisi kutoa hukumu juu ya mwenzao bila kufanya uchunguzi wa kina huku wakisema makamanda Mambosasa na Bwire pia wanatofautiana kauli zao juu ya tukio hilo.