Njoolay: Ma-RC, Ma DC wanahitaji semina elekezi

Mkuu wa zamani wa mikoa kadhaa nchini, Daniel Ole Njoolay (kulia) akizungumza na mwandishi wa gazeti hili, Moses Mashalla katika mahojiano maalumu yaliyofanyika jijini Arusha hivi karibuni. Picha na Mpigapicha Wetu

Muktasari:

Akizungumza na Mwananchi katika mahojiano maalumu hivi karibuni, mkuu wa mkoa mstaafu katika mikoa ya Arusha, Mwanza na Rukwa, Daniel Ole Njoolay, anatoa angalizo kuwa pamoja na mamlaka makubwa waliyo nayo viongozi hao, hatua hizo zinatakiwa kuchukuliwa kwa uangalifu.

Katika mkakati wa kurejesha dhana ya utawala bora na nidhamu katika uwajibikaji tumeshuhudia baadhi ya wakuu wa mikoa na wilaya wakiwawajibisha baadhi ya watendaji kwa kuwachukulia hatua za kinidhamu ikiwa ni pamoja na kuwasimamisha kazi.

Katika mlolongo huo, tumeshuhudia viongozi hao wakiwachukulia hatua kali baadhi ya watendaji kwa kuwatia ndani na kuzua sintofahamu na malalamiko mengi ya ukiukaji wa utawala bora.

Akizungumza na Mwananchi katika mahojiano maalumu hivi karibuni, mkuu wa mkoa mstaafu katika mikoa ya Arusha, Mwanza na Rukwa, Daniel Ole Njoolay, anatoa angalizo kuwa pamoja na mamlaka makubwa waliyo nayo viongozi hao, hatua hizo zinatakiwa kuchukuliwa kwa uangalifu.

Ole Njoolay anasema majukumu ya wakuu wa mikoa na wilaya ni makubwa kwa kuwa wao ndiyo wawakilishi wa Rais katika maeneo husika na hivyo majukumu hayo yanapaswa kuangaliwa kwa umakini.

Anasema kitendo cha kuwapo kwa matukio makubwa ya baadhi ya wakuu wa wilaya na mikoa kukamata baadhi ya watumishi wa Serikali na wengine wa kisiasa na kuwatia ndani kinatokana na viongozi hao kutopewa semina elekezi na kutojua mipaka yao ya kazi.

“Sisi zamani tulikuwa na bahati ya kupewa mafunzo ya kutueleza majukumu na mipaka yetu ya kazi, tulipata mafunzo haya hapa nchini na hata huko nchini Ireland, kwenye uongozi wetu hapakuwapo matukio makubwa kama ya sasa,” anasema Ole Njoolay ambaye pia aliwahi kuwa balozi wa Tanzania nchini Nigeria.

“Huenda wa sasa hawajapata semina elekezi, hizi semina elekezi zinasaidia sana kumfanya kiongozi wa umma kuongoza badala ya kutawala. Kuna tofauti kati ya kuongoza na kutawala. Kuongoza ni kuonyesha njia, kushawishi, kuheshimu watu na kushirikisha,” anasema.

Akitoa mfano, Ole Njoolay anasema anakumbuka katika kipindi cha miaka 16 alichohudumu kama mkuu wa mkoa, aliwahi kuitumia mara moja sheria ya tawala za mikoa kwa kumweka ndani mfanyabiashara mmoja jijini Mwanza wakati akiwa mkuu wa mkoa.

Bila kumtaja, anasema mfanyabiashara huyo alikaidi kuwalipa mishahara watumishi wake waliokuwa kisiwani wakivua samaki.

Anasema aliamuru kukamatwa kwa mfanyabiashara huyo baada ya watumishi wake kuandamana hadi ofisini kwake kulilia malipo yao, lakini alipompigia simu alimdharau na kumjibu kwamba hawezi kufika mpaka amtumie ndege kwa kuwa yuko mbali.

“Wale watumishi walifika ofisini kwangu na kulalamika hawajalipwa mishahara yao kwa zaidi ya miezi mitatu na wanaishi kisiwani bila hata chakula, nikaomba namba ya simu ya tajiri yao nilipompigia akanijibu kwamba wewe ni nani? Nikamwambia mimi ni mkuu wa mkoa, akaniuliza tena mkuu wa mkoa wa wapi? Nikamwambia Mwanza, ndipo akanijibu yupo mbali nimtumie ndege. Anajibu hayo kumbe yupo hapohapo Mwanza, ndipo nikaagiza akamatwe,” anasema Ole Njoolay

Anasimulia kwamba baada ya kukamatwa aliagiza mfanyabiashara huyo afikishwe ofisini kwake ambapo alipowasili alimhoji kuhusu madai hayo na mfanyabiashara huyo alikiri na akasekwa mahabusu na alipotoka alilipa mishahara yote ya watumishi wake.

Hata hivyo, anasema pamoja na kuwapo sheria hiyo, anashauri kuwa ni vyema Serikali ya Awamu ya Tano ikatoa semina elekezi kwa viongozi mbalimbali, hususani wakuu wa mikoa na wilaya ili kuwafanya watambue mipaka yao ya kazi.

“Kitu ninachokisisitiza hapa siwalaumu wakuu wa wilaya au mikoa, ila nashauri Serikali itoe semina elekezi kwa kuwa ni muhimu sana watambue mipaka ya majukumu yao. Serikali lazima ione umuhimu wa kuwapa semina elekezi,” anasisitiza Ole Njoolay

Kuhusu dawa za kulevya

Akizungumzia vita vya dawa ya kulevya nchini, Ole Njoolay anaipongeza Serikali kwa kujitoa kupambana nayo, lakini ingekuwa ni yeye asingetumia njia ya kutaja majina ya watuhumiwa hadharani, bali angeviita vyombo vya ulinzi na usalama na kuvikabidhi orodha ya washukiwa ili iweze kufanyiwa kazi kwa kuwachukulia hatua.

“Hivi ni vita vya kila mtu, napongeza hatua hii lakini mimi nisingefanya kama ilivyofanyika, ningeipata ile orodha ningeviita vyombo vya ulinzi na usalama na kuwakabidhi na kutaka kujua wanachukua hatua gami,” anasema Ole Njoolay.

“Ukitangaza namna hiyo ni kama tayari umeshawahukumu, watakaochambua na kuthibitisha kwamba huyu mtu ni mhalifu au si mhalifu ni Mahakama na ukimtangaza hadharani halafu vithibiti visipojitosheleza je, utamsafishaje,” anahoji

Kuhusu idadi ya Watanzania wanaokamatwa nje ya nchi, Njoolay anasema wakati akiwa balozi nchini Nigeria hakushuhudia matukio mengi.

Anasema alipata taarifa za kukamatwa kijana mmoja wa Kitanzania katika Jimbo la Lagos na akafikishwa mahakamani na kisha kuhukumiwa kifungo cha mwaka mmoja, lakini baadaye alipata msaada wa mawakili na kuachiwa huru na baada ya hapo ubalozi ulimsaidia kumtafutia usafiri wa kumrudisha nyumbani.

“Kijana huyu alikamatwa akiwa na dawa nyingi za epherdrine huko Nigeria ambayo yanatafsiriwa kama dawa za kulevya hapa nchini, lakini pia kuna binti mwingine wa Kitanzania alikamatwa akiwa Ivory Coast, niliondoka kesi yake bado inaendelea,” anasema.

Utumbuaji majipu

Kuhusu dhana ya utumbuaji majipu, Ole Njoolay anasema ikitumika vizuri siyo mbaya kwa kuwa mara nyingine kumekuwapo na ucheleweshaji katika kuwachukulia hatua baadhi ya watumishi wa Serikali ambao wamekuwa wakienda kinyume na maadili yao ya kazi.

Anasema dhana ya utumbuaji majipu inasaidia kuwafanya baadhi ya watumishi wa Serikali ambao ni wazembe kuamka endapo walikuwa wamelala na kufanya kazi kwa bidii lakini hata hivyo, anasisitiza taratibu na sheria za kuwawajibisha zifuatwe.

“Utumbuaji majipu unasaidia sana kuwaamsha hawa watumishi wazembe wafanye kazi kwa bidii hii, dhana ikitumika vizuri siyo mbaya cha muhimu taratibu za kiutumishi zitumike katika kuwatumbua,” anasisitiza Ole Njoolay.

Mkuu huyo wa zamani wa mkoa anasema hana shida na utumbuaji majipu kwa wateule wa kisiasa, lakini kwa watumishi wa umma ni muhimu kuzingatia sheria, kanuni na taratibu kwa kuwa wanaweza kusimamishwa kimakosa halafu wakaishtaki Serikali na ikajikuta inaingia gharama kuwalipa fedha nyingi na kuliingizia Taifa hasara.

Kuhamia Dodoma

Katika mpango wa kuhamia Dodoma, Njoolay anauunga mkono kwa asilimia 100, lakini anatoa angalizo kwamba Serikali ni lazima izingatie bajeti wakati ikilenga mpango huo.

“Tuhamie Dodoma kwa kuzingatia bajeti, tuwe tunaweka kwenye bajeti za wizara kila mwaka lakini pia tuangalie na kasi yetu kwani unaweza kufanya jambo kwa malengo mazuri lakini kasi ikawa shida,” anasema.

Tanzania ya Viwanda

Kuhusu mpango wa Serikali kutekeleza uchumi wa viwanda, Ole Njoolay anaipongeza Serikali kwa kulenga uchumi wa kati na kufafanua kuwa uchumi wa viwanda unapaswa kuangalia vizuri sekta binafsi kwa kuwa ndiyo inaajiri asilimia 67 ya nguvu kazi ya Taifa.

“Tusijisumbue na wala kujidanganya kwamba tunaweza kuyafufua mashirika ya umma, cha muhimu Serikali itengeneze mazingira rafiki kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi,” anasema.

Kwa ujumla, balozi huyo mstaafu  anasema Serikali ya Awamu ya Tano imefanya mambo makubwa kwa kipindi kifupi cha mwaka mmoja, jambo ambalo tawala zilizopita hazikuweza kulifanya.

Akitaja mafanikio hayo, anasema imefanikiwa kukusanya kodi, kupambana na rushwa na ufisadi, kubana matumizi na ubunifu wa kubadilisha matumizi ya fedha na kuzielekeza maeneo nyeti.

Hata hivyo, anasema changamoto kubwa anayoina ni upande wa suala la utawala bora.