Catalonia kufanya uamuzi mzito

Muktasari:

  • Bunge litafanya kikao chake Jumanne ambacho Puigdemont anatarajiwa kutoa mwelekeo kuhusu “hali ya sasa ya kisiasa.”

Wahispania leo wameamkia wiki iliyojaa sintofahamu kisiasa huku Rais wa jimbo la Catalonia Carles Puigdemont akitarajiwa kutangaza uhuru hivyo eneo hilo kujitenga kutoka Hispania.

Hofu zaidi ni kesho Bunge la Catalonia litakapokutana kuamua hicho walichokiita kujitangazia uhuru.

Puigdemont, ambaye ni kiongozi wa wanaharakati wanaopigania Catalonia kuwa huru aliaapa wiki iliyopita kutangaza uhuru baada ya kutokea mgawanyiko na kura ya maoni tata iliyofanyika Oktoba Mosi akisema ilielezea utashi halisi wa wananchi.

Hata hivyo, serikali yenye makao makuu yake Madrid imesisitiza kwamba kura hiyo ilikuwa batili na matokeo yake hayatambuliwi.

Msuguano kati ya serikali kuu yenye makao yake Madrid na ya Catalonia ambayo makao yake ni Barcelona umeitumbukizi Hispania katika mgogoro mkubwa wa kisiasa katika miongo minne iliyopita, tangu nchi ilipokuwa kwenye kipindi cha mpito kuelekea kwenye demokrasia.

Waziri Mkuu wa Hispania Mariano Rajoy aliapa Jumamosi iliyopita kutumia kila aina ya chombo alichonachom kisheria kuzuia uwezekano wa Catalonia kumeguka na kuwa taifa huru ikiwa ni pamoja na panoja na kutumia kifungu cha Katiba ambacho hakijawahi kutumika cha kusitisha mamlaka ya Catalonia.

"Tutazuia eneo hilo kujitangazia uhuru. Katika hili, naweza kuwaeleza kwa uwazi kabisa, kwamba haitatokea. Kwa hakika tutatumia uamuzi wowote tulioruhusiwa kisheria kadri mambo yatakavyokuwa yanajifunua," Rajoy aliliambia gazeti la El Pais katika mahojiano maalumu mwishoni mwa wiki.

"Hali ilivyokuwa ni kwamba hakukuwa na haja ya kutumia hatua kali, lakini kwa sasa haja hiyo ipo ya kufanyia marekebisho."

Katikati ya wiki iliyopita yalifanyika maandamano makubwa maeneo mbalimbali ya Catalonia kuunga mkono harakati za kujitenga na kujitangazia uhuru lakini mwishoni mwa wiki, yalifanyika maandamano katikati ya jiji la Barcelona ya watu wanaopigania umoja wa kitaifa.

Wafuasi wa chama cha Popular Unity Candidacy (CUP) kinachoongozwa na Puidgemont walitishia kuitisha Bunge leo kupitisha uamuzi wa kujitangazia uhuru lakini Mahakama Kuu ilitoa amri Bunge lisiitishwe.

Msemaji wa Bunge la Catalonia ameiambia CNN kwamba Bunge litafanya kikao chake Jumanne ambapo Puigdemont anatarajiwa kutoa mwelekeo kuhusu “hali ya sasa ya kisiasa.”