Nape auza sera ya Magufuli kwa Yutong

Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Nape Nnauye

Muktasari:

Akizindua aina mpya ya basi la Yutong F12 Plus jijini Dar es Salaam juzi, Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Nape Nnauye aliwataka viongozi wa kampuni hizo kuona umuhimu wa kujenga kiwanda nchini cha kuunganisha magari hayo.

Dar es Salaam. Kiwanda cha magari ya Yutong cha China kwa ubia na kampuni ya Benbros Motors Ltd, kimeshauriwa kuunga mkono jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano, Chini ya Rais John Magufuli kwa kujenga kiwanda cha kuunganisha magari hayo nchini.

Akizindua aina mpya ya basi la Yutong F12 Plus jijini Dar es Salaam juzi, Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Nape Nnauye aliwataka viongozi wa kampuni hizo kuona umuhimu wa kujenga kiwanda nchini cha kuunganisha magari hayo.

“Tunahimiza Yutong kwa ubia na Benbros kuanza kuunganisha magari haya nchini, hiyo itasaidia kuunga mkono jitihada za Serikali kujenga nchi ya viwanda,” alisema Nape.

Meneja Mkuu Mauzo wa Benbros, Albert Currusa alisema aina hiyo mpya ya mabasi ilianza kutengenezwa 2014 na kukamilika Mei, lakini uongozi haukuruhusu kuingia sokoni kwa kutaka kujiridhisha zaidi.

“Mei baada ya kukamilika hawakutaka kuingiza sokoni kwa sababu walitaka kujiridhisha kwanza na usalama na uimara wake, basi linapokamilika lazima liangaliwe likigongwa mbele, nyuma au pembeni usalama wa abiria ukoje, baada ya kujiridhisha sasa mwali ametolewa,” alisema Currusa.

Alisema kampuni hiyo imechukua wazo la Waziri Nape, hivyo watakaa kuona namna linavyoweza kutekelezwa.

Awali, Meneja wa Yutong nchini, Kim Zing alisema Yutong zenye injini mbele ziliingia soko la Tanzania kwa mara ya kwanza 2009/10 na hadi sasa mabasi 500 yapo kwenye soko la Afrika Mashariki.

“Yutong ni kampuni kubwa duniani ya utengenezaji mabasi, 2015 tuliuza magari 67,000 duniani yenye thamani ya Dola 4 bilioni za Marekani na kuwa kampuni pekee ambayo mauzo yake yanakua kwa asilimia tisa kwa mwaka,” alisema Zing. Alisema asilimia 10 ya mauzo yote wanairejesha kuhakikisha wanaboresha maendeleo.

Alisema kuanzia Novemba 25 hadi Desemba 25, wateja wataruhusiwa kupeleka mabasi yao kukaguliwa na kufanyiwa matengenezo bure na basi jipya linaponunuliwa litakuwa chini ya uangalizi kwa miaka miwili au kilomita 200,000.

Uzinduzi huo ulihudhuriwa na baadhi ya wabunge wa Tanzania na Zambia na wamiliki wa magari nchini.