Mwakyembe akumbushwa misingi ya sheria

Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Harrison Mwakyembe

Muktasari:

  • Katika barua yake kilichomwandikia Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Harrison Mwakyembe, EALS kimesema uhuru wa mwanasheria ni nguzo muhimu kwa sheria za kimataifa ambao umekuwa ukijadiliwa kwenye mikutano mbalimbali ya kimataifa.

Dar es Salaam. Chama cha Wanasheria Afrika Mashariki (EALS), kimesema  wanasheria wanatakiwa wapewe uhuru, wasiingiliwe na Serikali kama ilivyo kwa nchi nyingine kwani kuingilia ni sawa na kuvunja sheria za nchi.

Katika barua yake kilichomwandikia Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Harrison Mwakyembe, EALS kimesema uhuru wa mwanasheria ni nguzo muhimu kwa sheria za kimataifa ambao umekuwa ukijadiliwa kwenye mikutano mbalimbali ya kimataifa.

Barua iliyoandikwa na Rais wake, Richard Mugisha inatokana na kauli ya Dk Mwakyembe hivi karibuni kwa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), akidaiwa kutishia kukifuta kwani imeanza kuingilia siasa.

EALS kilimtaka Dk Mwakyembe kuacha kuingilia uchaguzi TLS. Uchaguzi wa chama hicho unatarajiwa kufanyika Machi 18

Rais wa TLS, John Seka alisema chama chake kimefurahishwa na barua hiyo kwa waziri na kwamba, nao pia wanafanya taratibu za kumuona ili kujadili mustakabali wa chama hicho.

Wagombea waliojitokeza kuwania urais wa chama hicho ni Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, Victoria Mandari, Francis Stola, Godwin Mwapongo na Lawrence Masha.