Mume aliyemuua mkewe Uingereza ahukumiwa kifungo cha miaka 23 jela

Muktasari:

Kema Salum (39), Mtanzania aliyetuhumiwa kumuua mkewe, Leila Mtumwa kwa kumchoma visu mara 49 sehemu mbalimbali mwilini amehukumiwa kifungo cha miaka 23 jela


London, Uingereza. Kema Salum (39), Mtanzania aliyetuhumiwa kumuua mkewe, Leila Mtumwa kwa kumchoma visu mara 49 sehemu mbalimbali mwilini amehukumiwa kifungo cha miaka 23 jela.

Salum alikiri kumuua mkewe mahakamani katika nyumba waliyokuwa wakiishi eneo la Haringey lililopo Kaskazini mwa London.

Awali, Salum  alikuwa amehukumiwa kifungo cha maisha  katika mahakama ya Old Bailey.

Ilielezwa mahakamani kuwa siku ya tukio Leyla alikuwa ametoka kwenye starehe na baadhi ya marafiki zake lakini akarejea asubuhi na Salum kuanza kumchoma visu.

Salum alijitetea mahakamani kuwa alifanya kitendo hicho kutokana na wivu wa mapenzi.

Kabla ya kumshambulia kwa visu inadaiwa alimkaba shingoni na baadaye akaelekea jikoni alikochukua kisu na kuanza kumshambulia.

Maelezo yaliyotolewa mahakamani yameonyesha kuwa Salum ambaye aliwasili London miezi michache iliyopita, alimshambulia Lelya maeneo mbalimbali ikiwamo shingoni huku mtoto wao wa miaka 12 akipiga kelele akimtaka asiendelee kufanya hivyo.

Alipokamatwa  baada ya tukio hilo aliwaeleza polisi alifanya hivyo ili kujihami.

Katika hatua za awali za usikilizaji wa kesi hiyo, alikana kuhusika na mauaji na baadaye wakati kesi hiyo ikiendelea alibadili msimamo wake na kukiri.

Wawili hao walifunga ndoa mwanzoni mwa 2017 na kwenda kuishi Uingereza.

Mama wa marehemu, Hidaya Mtumwa alitungiwa wimbo na mwanamuziki Pepe Kalle alipokuwa nchini Tanzania miaka ya 1990. Wimbo huo wa Hidaya ulikuwa maarufu kwa wapenzi wa muziki kote Tanzania.

Akiwa miongoni mwa wanamuziki kutoka DR Congo, Pepe Kalle amewahi kufanya ziara nchini mara kadhaa na kundi lake la Empire Bakuba lililokuwa na wanamuziki wengine mahiri kina Papy Tax, Bileku Mpasi na wengineo wakiwamo wacheza shoo wawili wafupi, Emoro na Jolie Bebe. Pepe Kalle, alifariki dunia mwaka 1998.