Maveterani wamkosoa Mugabe, mkewe

Muktasari:
Wasema Rais Mugabe anaposema maveterani au wapigania uhuru ambao wanaendelea kutumika jeshini hawana jukumu ndani ya Zanu PF hawawezi kusema anaongopa, lakini ni kwamba amesahau tulivyokubaliana kwamba bunduki itawaweka huru watu na kulinda kura.
Harare, Zimbabwe. Chama cha Maveterani wa Vita vya Ukombozi wa Zimbabwe (ZLWVA) kimesema mashambulizi yanayoelekezwa kwa makamu wa rais anayepigwa vita Emerson Mnangagwa na Waziri wa Maveterani aliyeondolewa Tshinga Dube hayawalengi wao tu bali maveterani wote.
Akizungumza katika mkutano wa waandishi wa habari jijini Harare, Katibu Mkuu wa ZLWVA, Victor Matemadanda amesema Rais Robert Mugabe na mke wake Grace hawawezi kudai kuwa wana uwezo wa kuwadhibiti wapigania uhuru na chama cha Zanu PF akisema maveterani hao walikwenda vitani kwa hiari yao na siyo kujiunga na watu.
Alisema kauli zinazotolewa na Rais Mugabe kwamba maveterani ambao bado wako jeshini hawakuwahi kuwa na jukumu lolote katika chama tawala cha Zanu PF zimeelekezwa kusiko.
"Mashambulizi dhidi ya Makamu wa Rais Mnangagwa na Bwana Tshinga Dube siyo tu kwamba yameelekezwa kwao peke yao bali maveterani wote kwa ujumla wao. Tunajua kwamba watajaribu hata kuvuruga mfumo wa jeshi lakini hawawezi kuvuruga historia tuliyoijenga,” amesema.
Matemadanda amesisitiza kwamba ni maveterani hao walioshawishi umma wa watu kukubali kuunga mkono mapambano ya silaha na kwamba hawakupigania uhuru kwa ajili ya inayoitwa familia ya kwanza kufurahia wakati Wazimbabwe wangi wakigalagala kwenye umaskini wa kutupwa.
Alisema hakuna hata mtu mmoja, akiwemo Rais Mugabe, aliyemiliki Zanu PF kwa kuwa chama hicho kilikuwa mali ya majeshi ya wapigania uhuru ZIPRA na ZANLA pamoja na wananchi wa Zimbabwes.
"Hakuna mtu mwenye mamlaka ya kusema anamiliki Zanu PF. Wanaweza kusema wanamiliki Zanu Mwenje au Zanu nyingine lakini Zanu PF ni ya kila mmoja. Ikiwa kuna watu wanadhani wanaweza kutupokonya Zanu PF hao wanafanya masihara.
"Rais Mugabe anaposema maveterani au wapigania uhuru ambao wanaendelea kutumika jeshini hawana jukumu ndani ya Zanu PF siwezi kusema anaongopa; lakini ni kwamba amesahau tulivyokubaliana kwamba bunduki itawaweka huru watu na kulinda kura.”