Mtoto wa rais ahukumiwa kifungo jela

Muktasari:

Mbali ya kutumikia kifungo cha miaka mitatu jela, pia mali zake zilizoko Ufaransa kama vile magari ya kifahari na jumba la kifahari lililoko eneo la Avenue Foch zitataifishwa. Kadhalika amepigwa faini ya euro 30milioni

Paris, Ufaransa. Mahakama moja nchini Ufaransa imemhukumu kifungo cha miaka mitatu jela makamu wa rais wa Guinea ya Ikweta, Teodorin Obiang Nguema katika kesi ya ufisadi iliyojulikana kama “umiliki wa mali haramu.”

Hata hivyo Teodorin mwenye umri wa miaka 48 na ambaye ni mtoto wa kiongozi wa muda mrefu Rais Teodoro Obiang Nguema hakuwepo mahakamani wakati inatolewa hukumu hiyo.

Mbali ya kutumikia kifungo cha miaka mitatu jela, pia mali zake zilizoko Ufaransa kama vile magari ya kifahari na jumba la kifahari lililoko eneo la Avenue Foch zitataifishwa. Kadhalika amepigwa faini ya euro 30milioni.

Serikali ya nchi hiyo ilijaribu kuzuia kesi hiyo kwa misingi kwamba ilikuwa kinyume cha sheria za kimataifa lakini ilikwama. Desemba 2016, Mahakama ya Kimataifa ya Haki za Binadamu yenye makao yake Hague ilitupilia mbali maombi ya Equatorial Guinea kusitisha kesi hiyo.

Teodorin alikuwa ameshtakiwa kwa kutumia fedha za serikali kufadhili maisha ya anasa katika jiji la Paris.

Miongoni mwa mali alizopata kwa kutumia fedha hizo ni kununua majengo ya kifahari kwa zaidi ya dola 100 milioni za Marekani, boti yenye urefu wa mita 76, na magari mengi ya kifahari kama vile Bugatti, Ferrari na Rolls Royces ambavyo vyote sasa vinataifishwa.

Babake Teodoro Obiang Nguema, amekuwa mamlakani tangu mwaka 1979 na ndiye rais wa Afrika aliyetawala kwa muda mrefu zaidi.