Mke wa Azory Gwanda ajifungua, amlilia mumewe

Anna Pinoni, ambae ni mke wa mwandishi wa kujitegemea wa MCL, Azory Gwanda akiwa na mtoto wake Gladness nyumbani kwake mkoani Pwani jana.

Muktasari:

Anna Pinoni (36), alijifungua mtoto wa kike Jumanne iliyopita katika Kituo cha Afya Kibiti na kumpa jina la Gladness.

Kibiti. Mke wa mwandishi wa habari wa kujitegemea wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Azory Gwanda aliyetoweka tangu Novemba 21 mwaka jana wilayani Kibiti mkoani Pwani amejifungua akitoa wito mumewe aachiwe ili walee mtoto pamoja.

Anna Pinoni (36), alijifungua mtoto wa kike Jumanne iliyopita katika Kituo cha Afya Kibiti na kumpa jina la Gladness.

Akizungumza na wafanyakazi wa gazeti la Mwananchi waliomtembelea jana nyumbani kwake kumjulia hali, mama huyo alisema anaumia kwa kubeba jukumu zito la kulea mtoto bila baba yake kuwepo na kuiomba Serikali kusaidia ili mumewe apatikane.

“Ninaomba wale wanaojua wamemteka mume wangu wamwachie aje tusaidiane kulea mtoto, siwezi kumlea peke yangu. Naiomba Serikali isaidie mume wangu apatikane haraka,” alisema.

Wakati Azory akitoweka, alimwacha Anna akiwa na ujauzito wa miezi sita na mama huyo alisema tangu wakati huo amekuwa akisaidiwa na ndugu, jamaa na marafiki wa mumewe hadi alipojifungua.

“Nimejifungua kwa operesheni lakini ninaendelea vizuri na ninamshukuru Mungu madaktari wamenisaidia na wamenipatia huduma nzuri,” alisema.

“Nilitamani mume wangu awepo, nilitamani sana amuone mwanaye (bintiye) ila namwachia Mungu,” alisema Anna huku akiendelea kumnyonyesha mtoto wake.

Alisema tangu mumewe atoweke ni miezi mitatu sasa na hakuna taarifa mpya zenye matumaini kwake na kwamba, kila jua linapozama anaona giza nene likitanda bila ya kupatikana kwake.

“Sina taarifa yoyote, hali ni ileile jua linachomoza na linazama mume wangu haonekani. Naumia kwa kweli sijui hawa watoto nitawalea vipi nami sina kazi. Mume wangu ndiyo alikuwa tegemeo langu,” alisema.

Akizungumzia usalama wake na familia yake alisema uko vizuri kwa kuwa hajapokea vitisho vyovyote wala taarifa ya kuhatarisha usalama wao.

Paskazia Pinoni ambaye ni dada wa Anna aliishukuru Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd (MCL) kwa namna inavyoisaidia familia.

“Mke wa Azory anaumia, tunajitahidi sana kumtuliza lakini juzi sababu ya mawazo ya kupotea kwa mume wake presha ilipanda na hali ikawa mbaya, alikuwa akilia tu na kusema sasa itakuwaje na hawa watoto,” alisema.

Dainess James ambaye ni shemeji wa Azory alisema hakuna tishio la usalama ingawa juzi wakiwa hospitalini kuna watu wawili walikwenda nyumbani kwa Azory saa nane usiku wakiwa wamevaa makoti makubwa na mabuti. Alisema Paskazia ndiye aliyekuwa nyumbani muda huo na alisikia vishindo nje ya nyumba. Alizima taa na alipochungulia dirishani aliona wanaume wawili mmoja akiwa amesimama mlangoni na mwingine kwenye kona ya nyumba lakini baada ya muda waliondoka na hawakurudi tena.