Miezi sita utekelezaji wa bajeti, wabunge wataka kasi zaidi

Muktasari:

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti, Hawa Ghasia akiwasilisha taarifa bungeni hivi karibuni alisema katika kipindi cha nusu mwaka, Serikali imekusanya asilimia 44.4 tu ya mapato yote yaliyoidhinishwa na Bunge kwa mwaka mzima.

Dodoma. Ikiwa imepita miezi sita ya utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2017/18 baadhi ya wabunge wameishauri Serikali Kuu kuongeza kasi ya upelekaji fedha katika halmashauri kwa ajili ya miradi ya maendeleo.

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti, Hawa Ghasia akiwasilisha taarifa bungeni hivi karibuni alisema katika kipindi cha nusu mwaka, Serikali imekusanya asilimia 44.4 tu ya mapato yote yaliyoidhinishwa na Bunge kwa mwaka mzima.

“Kamati imebaini kuwa mwenendo wa makusanyo hadi kufikia nusu mwaka Desemba 2017, Serikali imekusanya mapato kwa asilimia 82.8 ya malengo yaliyowekwa katika kipindi hicho. Hata hivyo, kamati inaendelea kusisitiza Serikali iongeze juhudi za makusanyo katika kipindi kilichobaki,” alisema Ghasia.

Alisema hadi Desemba 31, 2017 Serikali ilikuwa imekusanya Sh12.955 trilioni na kati ya fedha hizo, mapato ya ndani yalikuwa Sh11.926 trilioni na mapato ya nje Sh1.028 trilioni.

Kwa upande wa matumizi, alisema Serikali ilitumia Sh12.955 trilioni. Kati ya fedha hizo, alisema matumizi ya kawaida yalikuwa Sh9.815 trilioni na ya maendeleo yalikuwa Sh3.140 trilioni.

Katika mwaka wa fedha wa 2017/18 Serikali ilipanga kukusanya na kutumia Sh31.711 trilioni, kati ya fedha hizo mapato ya ndani yalitarajiwa kuwa Sh28.68 trilioni na ya nje Sh3.029 trilioni.

Kwa upande wa matumizi, Serikali ilikusudia kutumia Sh31.711 trilioni ambazo kati yake Sh19.712 trilioni ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Sh11.999 trilioni ni kwa ajili ya matumizi ya miradi ya maendeleo.

Naibu Waziri Kivuli wa Fedha na Mipango ambaye pia ni mbunge wa Momba (Chadema), David Silinde akizungumzia makusanyo hayo, alisema yana changamoto tofauti na mwaka wa fedha uliopita wa 2016/17.

“Makusanyo yamekuwa ni nusu ya lengo ambalo tulitakiwa kukusanya kwa sababu mpaka sasa tumekusanya takribani asilimia 44 ambayo ni tofauti na mwaka jana kwa kuwa yameshuka zaidi,” alisema.

Silinde alisema uagizaji wa bidhaa umeshuka kwa asilimia 45 na mzunguko wa fedha pia umeshuka.

Alisema mfumuko wa bei bado upo kwa asilimia nne, lakini vitu vingine vimeendelea kushuka.

Silinde alisema fedha za ndani zilizokuwa zitumike katika miradi ya maendeleo zimeishia kufanya kazi ya kulipa mishahara na deni la Taifa.

Naibu waziri kivuli huyo alisema endapo Serikali haitapata fedha za mikopo na za washirika wa maendeleo hakuna jambo litakalofanyika, hivyo Serikali ijitathmini katika kipindi kilichobaki.

Mbunge wa Kaliua (CUF), Magdalena Sakaya alisema upelekaji fedha katika halmashauri ni mdogo unaosababisha kutokuwa na ufanisi katika utekelezaji miradi ya maendeleo.

“Kwa mfano, katika halmashauri ya Kaliua utekelezaji wa miradi ya maendeleo ni mdogo sana. Utakuta tunatekeleza miradi yetu kwa fedha kidogo inayotokana na mapato ya ndani,” alisema.

Alisema Rais John Magufuli ana mpango wa kuhakikisha anaipeleka nchi katika uchumi wa kati utokanao na viwanda, hivyo ni muhimu fedha za maendeleo zikaenda kama ilivyopangwa.

Alisema wakati wanambana Waziri wa Fedha na Mipango kuhusu fedha kutokwenda katika halmashauri aliwaambia wanalipa deni la Taifa.

Sakaya alisema kwa sababu wameshalilipa kwa muda mrefu, deni hilo limepungua na ni vyema Serikali ikajielekeza katika kupeleka fedha za miradi ya maendeleo.

Alishauri kuwe na vipaumbele vichache katika bajeti ijayo ambavyo Serikali itaweza kuvitekeleza na si kuweka miradi 100 wakati haiwezi kutekeleza hata 10.

Sakaya alisema fedha zote zinazokusanywa katika halmashauri na ngazi ya Taifa wahakikishe zinaenda katika miradi ya maendeleo.

Alisema katika halmashauri ya Kaliua waliambiwa fedha zitakazokwenda katika maendeleo zitakuwa ni asilimia 50 badala ya asilimia 60 za awali, mabadiliko ambayo alisema yanamsikitisha kwa sababu hakuna tathimini iliyofanyika.

Mbunge wa Rufiji (CCM), Mohamed Mchengerwa alisema bajeti ya 2017/18 ilikuwa na nyongeza ya fedha ikilinganishwa na ya mwaka 2016/17 iliyokuwa Sh29 trilioni hivyo matarajio ya wananchi ni kwamba zingekwenda kutatua kero zilizopigiwa kelele ikiwemo uhaba wa maji.

Mchengerwa alisema wamekuwa wakipigia kelele ujenzi wa barabara, lakini miradi mingi imesimama huku akiitaja barabara ya Nyamwage hadi Utete ambayo Serikali iliahidi kuitengeneza.

Mbunge wa Busega (CCM), Dk Raphael Chegeni alisema, “OC (matumizi mengineyo) imekwenda lakini si kama ilivyokuwa inatarajiwa kumekuwa na pengo kidogo kwa hiyo baadhi ya taasisi za Serikali na halmashauri hazijaweza kutimiza malengo kama ilivyotarajiwa.”

Alisema kuna miradi mingi inatekelezwa kwa fedha za ndani kama vile ujenzi wa reli, baadhi ya miundombinu, maji, utoaji wa elimu bila malipo na mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu, ambayo imechangia kutotekelezwa kwa bajeti kama ilivyotarajiwa.

Hali katika halmashauri

Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi imepokea ruzuku ya Sh3.7 bilioni kutoka Serikali Kuu kati ya zaidi ya Sh13 bilioni zilizopangwa kwa mwaka wa fedha 2017/18.

Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo, Eliud Mwaiteleke alisema fedha hizo ni sawa na asilimia 28.5.

Mwaiteleke alisema halmashauri imepokea kwa asilimia 100 fedha za maendeleo kupitia miradi ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf) na fedha za elimu bila malipo.

“Michango na misaada kutoka kwa wahisani na wadau wa maendeleo kutoka ndani na nje ya nchi imetuwezesha kutekeleza miradi ikiwemo ujenzi wa madarasa, ofisi na nyumba za walimu na vyoo katika shule za msingi na sekondari za umma,” alisema Mwaiteleke.

Alisema miradi ya sekta za afya na maji imetekelezwa kwa asilimia 50 kutokana na mapato ya ndani na michango ya wadau wa maendeleo.

Halmashauri ya Shinyanga imesema imepokea Sh10.318 bilioni hadi kufikia Desemba, 2017 fedha za ruzuku kutoka Serikali Kuu kati ya Sh43.241 bilioni katika bajeti ya mwaka 2017/2018.

Ofisa mipango wa halmashauri hiyo, Flora Nyanana bila kutoa mchanganuo, alisema fedha hizo ni kwa ajili ya mishahara, ruzuku ya matumizi ya kawaida na kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Alisema kwa vyanzo vya ndani hadi kufikia Desemba 2017 halmashauri ilikuwa imekusanya Sh496.976 milioni sawa na asilimia 28.2 ya makisio waliyotarajia ya kukusanya Sh1.759 bilioni.

Katika Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, Sh1.126 bilioni zimepokewa kati ya Sh6.6 bilioni ikiwa ni sawa na asilimia 17 ya fedha zilizoidhinishwa.

Meya wa Jiji la Arusha, Kalist Lazaro alisema katika miradi ya maendeleo, ruzuku ya Serikali Kuu ilikuwa Sh6.9 bilioni na zilizopelekwa ni Sh64.08 milioni pekee.

Alisema ruzuku kutoka kwa wahisani waliomba Sh8.2 bilioni lakini wamepata Sh920.3 milioni sawa asilimia 22.

“Katika mapato ya ndani jiji tulitenga Sh8.777 bilioni tumeshatoa Sh3.460 bilioni hivyo mpaka Desemba utekelezaji ni asilimia 31 kwa nusu mwaka wa fedha wa 2017/18, “ alisema.

Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Athuman Kihamia alisema bado mwaka haujafika mwisho hivyo wanaamini fedha zitapatikana.

Alisema wameshapokea na kukusanya Sh18.6 bilioni na wametumia Sh17.6 bilioni.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Monduli, Steven Ulaya alisema wamepokea asilimia 48 ya fedha kutoka Serikali Kuu, lakini hakuna mradi uliosimama.

Nyongeza na Ngollo John, Anthony Mayunga, Stella Ibengwe na Mussa Juma