Timu ya riadha kuondoka kesho

Dar es Salaam. Timu ya taifa ya riadha ya vijana itaondoka nchini kesho Jumanne kuelekea Nairobi, Kenya kwa basi tayari kushiriki mashindano ya dunia yatakayoanza keshokutwa Jumatano.

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Wilhelm Gidabuday timu hiyo haitakabidhiwa bendera ya taifa na badala yake wataikuta Kenya kwa balozi wa Tanzania nchini humo.

"Hafla ya kuiga timu ni gharama na RT tulishasema hatuna fedha ndizo sababu tuliomba msaada kutoka Serikali ikiashindikana, lakini niseme tu kwamba taratibu za kukabidhiwa bendera tumemuomba Balozi wetu nchini Kenya kutusaidia mara timu itakapowasili," alisema Gidabuday.

Alisema timu hiyo imekawia kuondoka nchini kutokana na sababu mbalimbali, lakini kubwa ni kutokamilika kwa pasipoti zao kwa wakati, pia 'booking' ya malazi wakiwa Nairobi inaanza kesho Jumanne.

"Hatukuwa na namna, pasipoti zao zimekamilika mchana huu, hivyo kesho wanariadha wetu wataondoka kwa basi ambapo tunatarajia kuingia Kenya siku hiyo hiyo," alisema mtendaji huyo mkuu wa RT.

Wanariadha, Winfrida Makenji na Shomari Mtalimu wataiwakilisha nchi kwenye mashindano hayo katika mbio za mita 1500 na 200, wamepata nafasi hiyo baada ya kufikia viwango kwenye mashindano ya Afrika ya kanda ya tano pamoja na wenzao 10 ambao RT imeshindwa kuwapeleka kwa madai ya ukata.