Kanda ya Ziwa kuamua ubingwa wa Simba

Muktasari:

  • Simba inayousaka ubingwa kwa msimu wa tano sasa, iliibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Majimaji mwishoni mwa wiki iliyopita, na sasa inakwenda Kanda ya Ziwa kwa michezo mitatu ambayo itatoa picha halisi ya mbio za ubingwa.

Dar es Salaam. Mwaka 2015 ilielezwa kuwa kura za Kanda ya Ziwa ndizo zitakazotoa Rais wa Tanzania kwa kuwa kuna mikoa minane, na ikawa, Simba inakwenda kanda hiyo kwa mechi zake za Ligi Kuu na kimsingi ndizo zitakazoamua nafasi yake ya kutwaa ubingwa ama la.

Simba inayousaka ubingwa kwa msimu wa tano sasa, iliibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Majimaji mwishoni mwa wiki iliyopita, na sasa inakwenda Kanda ya Ziwa kwa michezo mitatu ambayo itatoa picha halisi ya mbio za ubingwa.

Pamoja na kuwa na kibarua cha Kanda ya Ziwa, Simba itacheza na Prisons na Mbeya City kwenye Uwanja wa Taifa kabla ya kwenda kuumana na Kagera Sugar, Mbao FC na Toto Africans.

Kwa mujibu wa ratiba, Simba inayoshika nafasi ya pili ikiwa na pointi 48, itacheza na Kagera Sugar Machi 11, kabla ya kwenda Mwanza ambako Aprili 2 itaumana na Mbao kabla ya kumalizana na Toto Africans Aprili 8.

Ikiwa imedhamiria kutwaa ubingwa msimu huu, Simba haina budi kushinda michezo hiyo mitatu ya ugenini kama inataka kutimiza lengo lake.

Akizungumza na gazeti hilio, Kocha msaidizi wa Simba, Jackson Mayanja alisema kila mchezo una umuhimu kwakeo ili kufanikisha lengo la kutwa ubingwa.

“Tuna kazi moja, kuwa makini kwenye kila mchezo tunaocheza pasipo kujali unacheza na timu ipi, tukishamalizana na Mbeya City na Prisons mkakati wetu utaelekezwa Kanda ya Ziwa,” alisema Mayanja.

Akizungumzia mbinu ya kutumia washambuliaji watatu katika mchezo uliopita dhidi ya Majimaji, Mayanja alisema unalenga kuipatia mabao timu hiyo.

“Tunapoona kuna sehemu ina mapungufu lazima ubadilishe, ndio maana tuliamua kuwapanga washambuliaji watatu, tunahitaji matokeo mazuri kwenye michezo iliyobaki,” alisema Mayanja ambaye aliwahi kuifundisha Kagera Sugar na Coastla Union.