Mbunge ahoji fedha za ruzuku kwa halmashauri zitapelekwa lini

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashatu Kijaji 

Muktasari:

Mbunge huyo alitaka kujua utekelezaji wa suala hilo kama ambavyo liliidhinishwa na Bunge


Dodoma. Mbunge wa Viti Maalum (CCM) Leah Komanya amehoji Serikali itaanza lini kupeleka fedha za ruzuku katika halmashauri za wilaya kama ilivyoidhinishwa na Bunge.

Akiuliza swali hilo bungeni leo Septemba 4 2018, Komanya amesema pamoja na nia nzuri ya Serikali kudhibiti ulimbikizaji madeni lakini kumekuwa na changamoto katika utekelezaji wa shughuli za kila siku katika idara za halmashauri za wilaya zinazopokea ruzuku ya matumizi ya kawaida toka Serikalini. 

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashatu Kijaji amesema ruzuku kutoka Serikali Kuu hupelekwa kwenye halmashauri za wilaya kulingana na makusanyo halisi ya mapato ya mwezi husika.

“Hivyo Serikali itaendelea kupeleka fedha za ruzuku kwenye halmashauri zetu kutokana na makusanyo halisi kutoka vyanzo mbalimbali vya mapato,”amesema.

Katika swali la nyongeza, Komanya amehoji ni lini Serikali italipa madeni ya mwaka wa fedha 2017/18 ambayo yamehakikiwa mwaka 2018.

Akijibu swali hilo, Dk Kijaji amesema Aprili mwaka huu Serikali ilitoa Sh 43 bilioni kwa ajili ya kulipa madeni ya watumishi.