Mbowe atoa ya moyoni

Muktasari:

  • Miundombinu ya shamba hilo iliharibiwa kwa kinachoelezwa kuwa lipo karibu na chanzo cha maji.

Siku moja baada ya Mkuu wa Wilaya ya Hai, Galasius Byakanwa kuongoza uondoaji wa miundombinu katika shamba la Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, mwenyekiti huyo ameandika hivi ivi katika ukurasa wake wa Instagram:

"Najua haya yanatokea kwa sababu ya misimamo yangu ya kisiasa kwa sababu wa muelekeo wangu wa kisiasa na uthabiti na uimara wa chama ninachokiongoza, sasa mimi siwezi kuwa kondoo, nimesema siku zote, haya mambo ya duniani anayeyalipa ni Mungu, si mtawala yeyote yule.

“Hawatabadilisha mawazo yangu kwa kuharibu mali zangu, wanaweza kuharibu zote hata wakitaka roho yangu waichukue, waichukue tu lakini haitanisababisha nibadili msimamo wangu katika kuamini ninachokisimamia, ninachokipigania katika Taifa."

"Hakuna wingi wa mali ambao wataharibu utakaonifanya Mbowe nikapige magoti kama wengine wanavyopiga magoti, sitapiga magoti, nitasimama katika kweli na haki wakati wote wa maisha yangu, kwa hiyo hili halinishangazi kwa sababu najua gharama ya ninachokilipa.

“Wako watu wengi wamenipigia simu wakijaribu kunipa pole kunitia moyo, wengine wamejaribu kunitia hofu, wakiniambia Mwenyekiti Mbowe pengine uachane na siasa, nimewaambia sitoachana na siasa, nitafanya siasa, ilimradi ni siasa safi zenye kusimamia ukweli na haki nitasimama nazo."

Miundombinu ya shamba hilo iliharibiwa kwa kinachoelezwa kuwa lipo karibu na chanzo cha maji.