Mbowe atoa somo kwa CUF, kujenga ngome ya Chadema Tanga

Muktasari:

Madiwani wa CUF wamegawanyika, kundi moja lenye madiwani wanane linaongozwa na Mwenyekiti wa chama hicho Wilaya ya Tanga, Rashid Jumbe na jingine la madiwani 12 linaloongozwa na Mbunge wa Tanga, Mussa Mbarouk


Tanga. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema mgawanyiko uliopo baina ya madiwani wa CUF katika Halmashauri ya Jiji la Tanga utachelewesha maendeleo ya wananchi.

Madiwani wa CUF wamegawanyika, kundi moja lenye madiwani wanane linaongozwa na Mwenyekiti wa chama hicho Wilaya ya Tanga, Rashid Jumbe na jingine la madiwani 12 linaloongozwa na Mbunge wa Tanga, Mussa Mbarouk

Mbowe ambaye yupo mkoani hapa kwa ziara ya kukiimarisha Chadema, alisema mvutano wa madiwani hao unazorotesha maendeleo ya wananchi na kuinufaisha CCM.

“CCM inawaendesha madiwani wa CUF hapa Jiji la Tanga, wametunyong’onyeza Ukawa na kwa mwendo huu tegemeeni mwaka 2020 jimbo litarejea CCM,” alisema Mbowe na kusisitiza kuwa Ukawa (Umoja unaoundwa na vyama vya upinzani) hawatakubali kuona jimbo hilo likirejea kwa chama hicho.

Aliwashauri madiwani wa CUF ambao idadi yao ni kubwa katika Halmashauri ya Jiji la Tanga kukataa kugawanywa kwa maslahi ya CCM, badala yake wakae na kuelewana ili kuimarisha na kuupa nguvu upinzani.

Katika baraza la halmashauri hiyo, CCM ina madiwani 17 na CUF inao 20. Idadi hiyo inahusisha madiwani 24 wa kata na wengine ni wa viti maalumu na wabunge.

Mbowe aliyekuwa akizungumza na viongozi wa Chadema wa kata zilizopo jijini Tanga, alisema kutokana na mkoa huo kuwa ngome ya CCM, chama chake kimeamua kuelekeza nguvu hapa ili kuhakikisha upinzani unapata viti vingi vya ubunge na udiwani mwaka 2020.

Katika kuhakikisha nguvu za Chadema zinajikita Tanga, Mbowe aliyefungua matawi na ofisi ya mkoa, alisema mkutano wa kamati kuu na mkutano mkuu wa kanda ya kaskazini utakaokuwa na ajenda ya kuwachagua viongozi wa kanda hiyo utafanyika Tanga wiki hii.

Mbunge wa Momba, David Silinde aliwataka wakazi wa Tanga kuiga mfano wa mkoani Songwe anakotoka ambako kati ya majimbo sita yaliyopo, matatu yanaongozwa na Chadema.