Mbowe amshangaa Magufuli kumtema Nape, RC

Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe      

Muktasari:

Mbowe, ambaye ni mwenyekiti wa Chadema, alisema hayo jana wakati akiwasilisha maoni ya kambi ya upinzani kuhusu bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zake kwa mwaka 2017/18.

Dodoma. Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe ameeleza kushangazwa na kitendo cha Rais John Magufuli kutomuwajibisha mkuu wa mkoa anayetuhumiwa kuvunja sheria na kumvua uwaziri mbunge wa Mtama, Nape Nnauye kutokana na kosa la mteule huyo.

Mbowe, ambaye ni mwenyekiti wa Chadema, alisema hayo jana wakati akiwasilisha maoni ya kambi ya upinzani kuhusu bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zake kwa mwaka 2017/18.

Mbowe alisema Kambi ya Upinzani imeshangazwa na kitendo cha Rais Magufuli, kuendelea kumkingia kifua mkuu huyo wa mkoa katika matukio tofauti, ambayo ushahidi wa wazi unaonyesha matumizi mabaya ya madaraka na ukiukwaji wa haki za binadamu.

“Ni jambo la kusikitisha kuona Rais akimtoa kafara, waziri wake kwa gharama ya mkuu wa mkoa na ndiyo maana tunajiuliza kuna jambo gani lililojificha baina ya Rais na mkuu wa mkoa?” alihoji mbunge huyo wa Hai.

Alikuwa akirejea tuhuma za utajiri wa ghafla wa mkuu huyo wa mkoa, na kutumia magari ya kifahari ya watu aliowatuhumu kuhusika na biashara ya dawa za kulevya.

Pia kuhusika kwake kuvamia studio za kituo cha televisheni cha kampuni ya Clouds Media, akiwa na askari wenye silaha za moto, kwa ajili ya kulazimisha kirushe habari za kumchafua Askofu Josephat Gwajima wa Kanisa la Ufufuo na Uzima.

Alisema Serikali ya Awamu ya Tano imeonyesha dalili za wazi za kuvunja Katiba na kutupilia mbali misingi ya utawala wa sheria, demokrasia na uhuru wa habari.

Mbowe alisema tabia za viongozi wanaotumia madaraka yao vibaya haina budi kupingwa kwa nguvu zote.

“Kambi Rasmi ya upinzani inawataka viongozi waliopewa dhamana kuheshimu utu na haki za kila raia,” alisema

Aliyataja matukio ya ukandamizaji wa haki na demokrasia yaliyofanywa na Serikali kinyume cha Katiba na Sheria za nchi kuwa ni pamoja na kupigwa kwa marufuku kwa mikutano ya vyama vya siasa.

Mengine ni kupigwa marufuku kwa urushwaji wa moja kwa moja wa mijadala ya Bunge, kudhibiti wabunge wa upinzani wawapo bungeni, kuingiliwa kwa mhimili wa mahakama, kupuuza utawala wa sheria na uonevu unaofanywa na vyombo vya dola dhidi ya wananchi wa visiwa vya Unguja na Pemba.

Mbowe alisema kambi hiyo inaitaka Serikali kutekeleza ahadi hiyo kwa kurejesha tena mchakato wa Katiba mpya.

“Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapendekeza mchakato wa Katiba mpya urudishwe nyuma katika ngazi ya Bunge Maalum ili kujadili maoni ya wananchi katika Rasimu ya Pili ya Katiba iliyowasilishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba bila kuathiri maudhui ya maoni ya wananchi,” alisema.

Mbowe alisema tangu Serikali ya awamu ya tano iingie madarakani imekuwa ikijigamba uchumi wa nchi unakuwa kwa kasi ikilinganishwa na Serikali awamu zilizotangulia lakini kumekuwa na kilio kikuuu kwa upande wa wananchi kuhusu hali ya maisha kuendelea kuwa ngumu.

“Kilio hiki kinamaanisha kuwa ukuaji wa uchumi unaohubiriwa na Serikali haujawafikia wananchi ambao ndio wadau wakubwa wa nchi hii,”alisema.

Alisema Serikali haina mkakati wowote madhubuti wa kuinua uchumi kwa wananchi wanaoishi vijijini.

“Duniani kote hakuna nchi iliyowahi kufanikiwa kuingia kwenye uchumi wa viwanda kabla ya kupitia mageuzi ya kilimo,” alisema.

Alisema kinachoonekana ni kuwa serikali haikujiandaa na sera hiyo ya viwanda na inakurupuka kufanya mambo mbalimbali bila kuwa na mpango madhubuti wenye matokeo yanayopimika.

Mchanga wa dhahabu

Mbowe pia aliishauri Serikali ifanye mazungumzo ya kurejea mikataba kabla ya kutoa makatazo hadharani, kama ilivyokuwa katika sakata la mchanga kusafirishwa nje ya nchi kwa ajili ya kuchenjua ili kupata shaba na madini mengine ambayo hayawezi kutenganishwa kwenye vinu vya dhahabu.

“Mambo haya yanahitaji muda na mipango na kukurupuka kutakuja kulisababishia Taifa kupoteza imani ya wawekezaji wakubwa, hususan wa kimataifa,” alisema.