Mambo makubwa aliyofanya JPM Kanda ya Ziwa

Muktasari:

  • Katika ziara hiyo ya mikoa hiyo mitatu inayounda Kanda ya Ziwa pamoja na mikoa ya Shinyanga, Geita na Kagera, Rais Magufuli alitembelea, kukagua, kuweka mawe ya msingi na kuzindua miradi ya maendeleo pamoja na kuwahutubia wananchi katika mikutano ya hadhara.

Septemba 3, 2018, Rais John Magufuli alianza ziara ya siku nane katika mikoa ya Mwanza, Mara na Simiyu akitokea mkoani Geita alikokuwa kwa shughuli za kifamilia.

Katika ziara hiyo ya mikoa hiyo mitatu inayounda Kanda ya Ziwa pamoja na mikoa ya Shinyanga, Geita na Kagera, Rais Magufuli alitembelea, kukagua, kuweka mawe ya msingi na kuzindua miradi ya maendeleo pamoja na kuwahutubia wananchi katika mikutano ya hadhara.

Makontena ya Makonda

Kabla ya kuanza ziara hiyo, Rais Magufuli alikuwa nyumbani kwake Chato tangu Agosti 18, ambapo Agosti 30 alizungumza na madiwani, watendaji na viongozi wa Halmashauri hiyo na kutoa msimamo wake kuhusu sakata la makontena yaliyoingizwa nchini kwa jina la mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.

Katika hali iliyoonekana kumaliza mvutano kuhusu makontena hayo, Rais Magufuli alimtaka mteule wake huyo kulipa kodi na ushuru unaostahili kwa mujibu wa sheria.

Alisema sheria za nchi zinasema ni mtu mmoja pekee katika nchi mwenye dhamana ya kupokea msaada kwa niaba ya wananchi kwa mujibu wa sheria ya fedha, sheria ya madeni, sheria ya dhamana na ya misaada.

Ujenzi wa meli mpya

Septemba 3, Rais Magufuli alishuhudia utiaji saini wa ujenzi wa meli moja na ukarabati wa nyingine mbili zitakazohudumia katika Ziwa Victoria ikiwa ni miaka 22 tangu kuzama kwa meli ya MV Bukoba mwaka 1996.

Katika hafla hiyo, Kampuni ya Huduma za Meli Tanzania (MSCL) ilitiliana saini mikataba ya miradi hiyo na Kampuni ya Ms GAS Entec ya Korea Kusini, Suma JKT na Kangnam pia ya Korea Kusini zitakazotekeleza miradi hiyo yenye thamani ya zaidi ya Sh152 bilioni.

Kwa mujibu wa Kaimu Meneja wa MSCL, Eric Hakmisi, meli mpya inayojengwa inatarajiwa kukamilika baada ya miaka miwili na itakuwa na uwezo wa kubeba abiria 1,200, tani 400 za mizigo na magari madogo 20.

Katika hafla hiyo kabla ya kuhitimisha hotuba yake, Rais Magufuli alitoa muda wa wiki moja kwa Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe kukutana kumaliza tatizo la Kodi ya Ongezeko la Thamani (Vat) kwenye miradi ya ujenzi akisema inachelewesha na kukwamisha miradi.

Migogoro na minyukano

Septemba 5, 2018, Rais Magufuli alianza ziara ya siku nne mkoani Mara ambapo licha ya kuzindua na kutembelea miradi ya maendeleo na kuhutubia wananchi katika mikutano ya hadhara, pia alikemea tabia ya baadhi ya viongozi wa Serikali kugombana wakati wanapotumikia wananchi.

“Kwa nini mnagombana (viongozi) hadi kukwamisha shughuli za maendeleo? Tumieni vikao kujadili na kumaliza tofauti na changamoto zinazojitokeza miongoni mwenu wakati mnatekeleza wajibu wenu wa kutumikia wananchi,” alisema Rais Magufuli katika moja ya mikutano yake wilayani Tarime

Kwa kipindi kirefu, viongozi wa CCM katika wilaya za mkoa wa Mara, hasa Tarime wananyukana wao kwa wao kiasi cha kukwamisha utekelezaji wa miradi na ilani ya chama hicho tawala.

Kauli ya Rais iliwalenga Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Glorious Luoga na Mwenyekiti wa CCM wilayani humo, Daudi Ngicho pamoja na viongozi wa juu wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM).

Kwa upande mwingine upo mvutano baina ya Luoga na Mkuu wa Mkoa huo, Adam Malima juu ya kiwanda cha sukari ambapo kila mmoja akitaka kipewe jina tofauti na analolitaka mwenzake.

Maji, migogoro ya ardhi na uvuvi

Tatizo la majisafi na salama, migogoro ya ardhi na operesheni ya zana na uvuvi haramu ni kati ya vilio vikuu vilivyotawala ziara ya Rais katika mikoa ya Mwanza, Mara na Simiyu.

Miongoni mwa wilaya ambazo vilio vya wananchi kuhusu tatizo la maji vilihanikiza ni pamoja na Magu, Bunda, Musoma, Butiama na Serengeti.

Katika maeneo hayo yote, Serikali inatekeleza miradi mikubwa ya maji inayogharimu mabilioni ya fedha, lakini utekelezaji wake ama umekuwa duni au unasuasua huku wananchi wakiendelea kutaabika.

Baada ya kupokea malalamiko ya wananchi, Rais Magufuli alitumia mkutano wake wa hadhara wakati akizindua mradi wa maji wa Lamadi wilayani Busega mkoani Simiyu unaogharimu zaidi ya Sh12.8 bilioni kumwagiza Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Profesa Makame Mbarawa kuwashughulikia watendaji na wataalamu wa wizara waliosimamia miradi isiyo na tija.

Alimwagiza waziri huyo kutumia mamlaka yake kuwachukulia hatua ikiwemo kuamuru kukamatwa na kuwasweka mahabusu wanaokwamisha au kushindwa kusimamia miradi katika maeneo yao. “Nataka waziri (Profesa Mbarawa) ufanye uchunguzi kwenye miradi hii (ya maji) ikiwemo ya uchimbaji wa visima ambavyo havitoi maji licha ya kugharimu mabilioni ya fedha kwa sababu kabla ya utekelezaji utafiti na uchunguzi wa kitaalamu hufanyika kubaini kiwango cha maji chini ya ardhi,”

Kuhusu migogoro ya ardhi, aliwataka wakuu wa wilaya na mikoa yenye migogoro kuishughulikia na kuimaliza akionya kuwa endapo watashindwa kufanya hivyo hawatakuwa na sababu ya kuendelea kushikilia nyadhifa zao.

Akizindua barabara ya makutano-Natta-Mugumu inayounganisha wilaya za Butiama na Serengeti mkoani Mara yenye urefu wa kilomita 135, Rais Magufuli aliwataka viongozi kusikiliza na kutatua kero za wananchi ikiwemo migogoro ya ardhi.

Kuhusu zana na uvuvi haramu, kiongozi huyo alisisitiza msimamo wa Serikali kuendeleza operesheni ya kukamata na kuteketeza zana haramu za uvuvi ili kulinda samaki na rasilimali yake kwa faida ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Hata baada ya kupokea kilio na malalamiko kutoka kwa wananchi na viongozi wa kisiasa dhidi ya maofisa wanaounda timu za operesheni katika mikoa ya Kanda ya Ziwa, alitaka suala hilo lisigeuzwe mtaji wa kisiasa kwani bila hatua madhubuti samaki watatoweka Ziwa Victoria.

Alimmwagia sifa waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina kwa kusimamia vyema operesheni hiyo licha ya vikwazo kutoka kwa baadhi ya watu wakiwemo viongozi wenzake na kumhakikishia kuwa anaridhishwa na kazi inayofanyika na atamuunga mkono.

Rais alitumia mkutano wa hadhara katika mji wa Lamadi kumwagiza Mpina kuanza kuwashughulikia watendaji, wataalamu na viongozi ambao katika maeneo yao bado kuna vitendo vya uvuvi haramu.

Pia aliagiza kukamatwa na kushughulikiwa kwa wenyeviti wa vijiji na mitaa ambao vitendo vya uvuvi haramu vinagundulika katika maeneo yao kwa sababu ni lazima wanawafahamu wahusika.

Harambee ya papo hapo

Akiwa eneo la Nyamongo wilayani Tarime, Rais Magufuli aliendesha harambee ya papo hapo na kufanikiwa kukusanya zaidi ya Sh24 milioni kusaidia kutatua baadhi ya kero katika Sekondari ya Ingwe.

Uamuzi huo ulitokana na mmoja wa wanafunzi wa shule hiyo, Monica Bernard kuwasilisha kilio mbele ya Rais Magufuli kuhusu shule yao kukabiliwa na changamoto kadhaa ikiwemo uchache na ukosefu wa miundombinu, vifaa vya kufundishia na kujifunzia pamoja na samani kiasi cha wanafunzi watatu kulala kwenye kitanda kimoja.

Mwanafunzi huyo aliyezungumza baada ya kuruhusiwa na Rais, pia alisema shule hiyo yenye wanafunzi kuanzia kidato cha kwanza hadi cha tano ina upungufu wa walimu.

Katika harambee hiyo Rais alichangia fedha taslimu Sh5 milioni na kuagiza zitumike kutatua sehemu ya changamoto zilizotajwa na mwanafunzi huyo kulingana na maoni, mapendekezo na kipaumbele cha wanafunzi wenyewe.

Mchapakazi RC Mtaka

Licha ya mkoa wake kuwa kinara wa utekelezaji wa ilani ya CCM na ushirikiano kati ya viongozi wa Serikali na CCM ikifuatiwa na mikoa ya Singida, Dodoma na Pwani, Rais Magufuli alifichua kuwa mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka aliwekewa vigingi asiteuliwe kwa madai kuwa hafai hata ukuu wa wilaya.

Siri hiyo aliifichua Rais baada ya kuridhishwa na taarifa ya utekelezaji na utendaji wa Serikali mkoani Simiyu, ambapo alisema ushauri huo ulitolewa na wasaidizi wake wakati alipokuwa anajiandaa kufanya uteuzi wa wakuu wa wilaya na mikoa.