Majaliwa akagua ujenzi nyumba za askari Magereza

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akikagua eneo litakalojengwa nyumba 320 za makazi ya askari na maofisa wa magereza katika Gereza la Ukonga jijini Dar es Salaam. Picha na Bakari Kiango
Muktasari:
Majaliwa ametoa kauli leo katika Gereza la Ukonga alipotembelea gereza hilo kujionea maendeleo ya ujenzi wa nyumba 320 za askari na maofisa wa magereza.
Dar es Salaam. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewahakikisha askari wa magereza na majeshi mengine kuwa Serikali ina dhamira ya kuhakikisha wanapata makazi bora ili wafanye kazi kwa ufanisi.
Majaliwa ametoa kauli leo katika Gereza la Ukonga alipotembelea gereza hilo kujionea maendeleo ya ujenzi wa nyumba 320 za askari na maofisa wa magereza.
Amesema familia za askari zikiwa katika makazi bora inawasaidia askari kufanya kazi kwa weledi mkubwa na kwamba amefarijika kuona ujenzi huo unatekelezwa na Wakala wa Ujenzi wa Taifa (TBA).
“Sina shaka na kiwango cha TBA. Nina imani nao kama walivyojenga majengo mbalimbali ya Serikali,” amesema Majaliwa.
Majaliwa amesema amefanya ziara katika mikoa mbalimbali na amejiona jinsi nyumba za magereza zisizokidhi mahitaji ya watu kuishi.