VIDEO-MCL yaomba wadau kumsaidia mkewe Azory Gwanda

Muktasari:

Leo Februari 28,2018 Azory Gwanda ametimiza siku 100 tangu atoweke.

Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), imewaomba wadau, taasisi na watu wenye mapenzi mema kuiunga mkono kumchangia mke wa mwandishi wake wa kujitegemea Azory Gwanda aliyepotea katika mazingira ya kutatanisha.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Februari 28,2018 ambayo Azory ametimiza siku 100 tangu atoweke, Mkurugenzi Mtendaji wa MCL, Francis Nanai amesema Anna Pinoni ambaye ni mke wa Azory anahitaji msaada pamoja na watoto wake wawili.

“Kwa mwenye mapenzi mema ya kutusaidia atuunge mkono kwa kuchangia kwa lipa kwa TigoPesa namba 173333 ambayo pia ni Merchant Payment number (namba ya wakala)”

“Pesa hii itaratibiwa na MCL na itamfikia mhusika kwa wakati, kwa ukamilifu na kwa uwazi,”amesema Nanai.

Amesema kwa yeyote anayehitaji maelezo kuhusu mchango huo apige simu namba +255 22 5514222 aombe kuzungumza na meneja rasilimali watu au atume maoni kupitia barua pepe[email protected]

Nanai amesema MCL imeamua kusaidia kumkwamua mke wa Azory na watoto kwa kulipia gharama za mahitaji ya watoto ya shule na kulipia huduma za afya kupitia Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF).

“Tutampatia fedha za kumwezesha kuanzisha shughuli ya kiuchumi atakayoipenda na kuimudu na tutagharimia mahitaji mengine ya chakula na kujikimu,”amesema Nanai.

Amesema, “Wakati Azory anatekwa mkewe alikuwa mjamzito na tayari amejifungua mtoto wa kike aliyempa jina Gladness, tunamuomba Mungu ampe moyo wa subira, kuvumilia upweke, mawazo na mateso ya kutomwona mwenzi na baba wa watoto wake.”