Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tamasha la Fiesta lazuiwa Leaders Club

Muktasari:

Mkurugenzi wa manispaa ya Kinondoni, Aron Kagulumjuli amethibitisha kuzuiwa kwa tamasha la Fiesta kutokana na malalamiko ya wagonjwa na wamewataka waandaaji kuhamishia tamasha hilo viwanja vya Tanganyika Peakers vilivyopo Kawe, Dar es Salaam


Dar es Salaam. Manispaa ya Kinondoni imezuia tamasha la Fiesta kufanyika katika viwanja vya Leaders Club leo Jumamosi Novemba 24, 2018.

Kupitia barua inayosambaa katika mitandao ya kijamii manispaa hiyo imesema kuwa tamasha hilo limehamishiwa katika viwanja vya Tanganyika Peakers, badala ya Leaders Club.

Barua hiyo iliyoandikwa na ofisa utamaduni Manispaa hiyo jana Ijumaa Novemba 23, 2018 kwenda kwa waandaaji wa tamasha hilo, Clouds Media Group, ina kichwa cha habari kinachosema, kusitisha kibali cha kufanya Fiesta Leaders Club.

“Ofisi imepokea malalamiko ya wananchi na wagonjwa waliolazwa hospitalini kutokana na matangazo yaliyoambatana na muziki unaopigwa kwa sauti kubwa kutoka uwanja wa Leaders Club jambo ambalo linahatarisha afya za wagonjwa wakiwemo wa moyo,” inaeleza sehemu ya barua hiyo.

“Hivyo kwa barua hii nafuta kibali kilichotolewa Novemba 22, 2018 cha kufanya Fiesta uwanja wa Leaders na kuihamishia uwanja wa Tanganyika Peakers, Kawe.”

Katika ufafanuzi wake Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Aron Kagulumjuli amesema, “Tumelizuia (tamasha) kufanyika hapo kwani uhai wa watu ni muhimu kuliko hicho kinachotaka kufanyika.

“Jana tu walipokuwa wakitangaza hapo Leaders maeneo ya karibu kuna hospitali na watu wawili walizimia, sasa kwa njia hiyo hatuwezi kuruhusu furaha ya watu wengi ikawa majonzi kwa wengine.”

Amesema kwa hali ilivyo sasa hawawezi kuruhusu kufanyika kwa tamasha hilo viwanja vya Leaders hadi baadaye watakapojiridhisha ni salama kwa watu wengine.

Alipoulizwa kuhusu kuzuiwa kwa tamasha hilo meneja vipindi wa Clouds, Shafii Dauda amesema, “tutatoa taarifa baadaye (leo). Tusingependa kulisema hili sasa hivi.”