Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

VITA YA KAGERA: Mapambano yaendelea, majeshi ya Tanzania yauteka mji wa Arua-27

Muktasari:

Jana tulisimulia jinsi Profesa Yusuf Lule alivyoapishwa kuwa Rais wa Serikali ya mpito ya Uganda. Pia jinsi hafla ya kuapishwa kwake ilivyokuwa ni fupi. Baada ya kuapishwa, alitoa hotuba fupi, wakati mmoja akizungumza Kibaganda.

Hata hivyo, vita ilikuwa haijamalizika. Miji kama wa Arua bado ilikuwa haijakombolewa. Askari wa Tanzania walitaka kuhakikisha kuwa hakuna eneo limeachwa bila kuguswa. Endelea…

Wanajeshi wa Tanzania walipita maeneo mengi kuhakikisha kuwa hakuna askari wa Iddi Amin aliyebakia Uganda. Ingawa katika maeneo hayo wanajeshi wa Tanzania walipokewa vyema na raia wa Uganda, walionywa kuwa eneo la West Nile hali ilikuwa tofauti kwa sababu hiyo ilikuwa ni ngome ya Amin.

Kwa mujibu wa jarida la Africa Currents, watu wa eneo hilo walifikia hata hatua ya kuweka sumu kwenye mazao yao na kuwapa askari wa Tanzania.

Kitabu cha War in Uganda kinaandika kuwa katika viunga vya mji wa Masindi, askari watatu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania ambao walikula ndizi walizopewa na wakazi wa eneo hilo waliugua ghafla na kufariki dunia. Ilidaiwa kuwa walitia sumu hata kwenye maji ambayo walidhani Watanzania wangeyanywa.

Kiasi cha askari 10,000 wa Amin walikuwa wamekimbilia eneo hilo mara baada ya Kampala kukombolewa. Mabasi, malori na magari mengi ya kawaida yaliyoibwa maeneo mengi ya Uganda yalikutwa eneo hilo la West Nile. Mengi yalikuwa yametelekezwa njiani baada ya kuharibika.

Kwa majuma kadhaa, maofisa waandamizi wa Tanzania mjini Dar es Salaam na ofisi ya Jenerali David Musuguri mjini Entebbe walikuwa wakijadiliana namna ya kushughulikia tatizo la West Nile. Baadaye iliamuliwa kuwa eneo hilo litekwe kilomita moja baada ya nyingine.

Wanajeshi wa Tanzania walipofika maeneo hayo walikuta hoteli za kitalii za Paraa na Chobe zikiwa zimeporwa na wanajeshi wa Amin. Hoteli hizo zilikuwa katika hifadhi ya Kabelega. Askari hao walibomoa hata baadhi ya kuta za hoteli hizo ili wapate kuiba. Hata nyaya za umeme za majengo zilitolewa.

Maelfu ya askari wa Tanzania walisogezwa eneo hilo tayari kushambulia.

Siku moja kabla ya kushambulia, eneo hilo lilichunguzwa kwa uangalifu. Hata hivyo, wapiganaji na maofisa waandamizi hawakuona kama kulikuwa na watu ng’ambo ya pili ya Mto Pakwach kuelekea West Nile.

Baada ya kujiridhisha, askari wa Tanzania waliamua kuvuka mto kuelekea West Nile. Daraja la Pakwach halikuwa na ulinzi wowote wa askari wa Amin kama ilivyodhaniwa.

Baadaye JWTZ ikaona hakukuwa na sehemu nyingine yoyote ya Uganda ambayo ilihitaji uangalifu wa kijeshi kuliko maeneo yale ambayo tayari walikuwa wamepita. Ikiwa askari wa Amin walikuwa wamepanga kupigana, basi wangefanya hivyo kwenye Daraja la Pakwach.

Askari wa Tanzania walipofika eneo la Nebbi, walishangaa wakilakiwa kwa shangwe. Wakazi wengi waliwapa chakula na vinywaji, lakini askari hao walishaonywa wasile wala kunywa chochote wanachopewa huko.

Mapokezi hayo yalikuwa ni faraja kwa askari wa Tanzania na yaliendelea kuwa hivyo kijiji baada ya kijiji kuelekea Arua. Kote huko hakukuwa na dalili yoyote ya kuwapo kwa askari wa Amin isipokuwa risasi chache zilizosikika wakati wakivuka Mto Ora.

Lakini kuelekea Arua hakukuwa na dalili zozote za askari wa Amin. Arua ulikuwa mji wa mwisho wa Uganda kukombolewa na hapo ndipo ilipomalizikia vita iliyodumu kwa miezi minane.

Kulikuwa na taarifa zilizodai kuwa Amin alikuwa amejificha Arua. Zile sababu za awali za kujizuia kumuua Amin zilikuwa zimeshatoweka na sasa askari wa Tanzania walikuwa wanawaza jambo ambalo wengemfanya ikiwa watamtia mikononi mwao.

Kitabu cha War in Uganda kinasema kulikuwa na amri kuwa ikiwa Amin angepatikana akamatwe badala ya kuuawa. Maofisa wa Serikali mpya ya Uganda waliwaambia askari wa Tanzania kwamba walitaka Amin akamatwe ili ashtakiwe.

Brigedia Roland Makunda alikabidhiwa kazi ya kuitwaa Arua na kazi ya kuidhibiti njia ya kutoka Arua alikabidhiwa Brigedia Hemedi Kitete.

Katika kambi ya Bondo, kulitokea mapambano kidogo na askari wa Amin. Mashambulizi ya askari wa Amim yalikuwa ya mfululizo. Askari wa Tanzania walipojibu mapigo, milio ya risasi na mabomu ilisikika kama vile vita vimeanza upya.

Giza lilikuwa limeshaingia wakati magari ya wagonjwa yalipofika kuwabeba majeruhi. Askari sita wa Tanzania waliuawa katika tukio hilo na wengine 14 kujeruhiwa. Hakuna askari wa Amin aliyeuawa.

Asubuhi viunga vya mji wa Arua vikawa vimeshatekwa na Brigedi ya 206.

Brigedia Makunda akapata habari kuwa askari wa Amin walikuwa wamejichimbia katika Hoteli ya Rhino na kwamba raia wote walikuwa wameshakimbia. Alitaka kuilipua hoteli hiyo usiku huo.

Huo ndio ungekuwa mwisho wa vita kwa Brigedi ya 206 kwa sababu Brigedi ya Minziro ilikuwa inaondoka Arua kuelekea kwenye mpaka wa Uganda na Sudani.

Usiku askari wa Tanzania walishambulia kwa mabomu na kulipopambazuka Brigedi ya 206 ikaingia katika mji wa Arua. Hakukuwa na dalili zozote za kuwapo kwa Amin katika eneo hilo.

Mali za nyumba yake aliyoimiliki Arua zilikuwa zimeporwa sawasawa na zilivyoporwa za nyumba nyingine.

Nje ya nyumba hiyo liliegeshwa gari lake la kifahari aina ya Maserati. Askari wa Tanzania walijaribu kuliwasha lakini halikuwaka, wakaamua kuliacha.

Eneo hilo walikamatwa waliokuwa mawaziri wa Amin ambao ni Waziri wa Elimu, Brigedia Barnabas Kili; Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Luteni Kanali Michael Ambia na Ofisa Utawala na Mafunzo jeshini, Meja Vincent Yekoko. Watatu hao waliamua kuendelea kuwasubiri wanajeshi wa Tanzania mjini Arua badala ya kukimbilia Sudani au Zaire (DRC) pamoja na askari wengine wa Amin.

Mawaziri hao wa Amin walipohojiwa ndipo walipotoa siri kuwa Amin alikuwa ameshaikimbia Uganda. Alikwenda Arua mara baada ya Kampala kukombolewa na muda mfupi baadaye akaondolewa Uganda kwa ndege ya Libya na alipoondoka aliliacha jeshi lake bila uongozi na likageuka kuwa kundi la uporaji na mauaji.

Itaendelea kesho