Halmashauri Geita yaanza ujenzi wa shule 15

Muktasari:

Halmashauri ya mji wa Geita inatarajia kukamilisha hivi karibuni ujenzi wa shule mpya 10 za msingi na tano za sekondari ili kuhakikisha hakuna mtoto wa Geita ambaye anakosa nafasi ya kujiunga na shule ya msingi ama sekondari.

Arusha. Halmashauri ya mji wa Geita mkoani Geita inajenga shule mpya 10 za msingi na tano za sekondari ili kuhakikisha hakuna mwanafunzi anakosa nafasi ya kujiunga na shule ifikapo mwaka 2019.

Akizungumza na Mwananchi hivi karibuni, mkurugenzi wa halmashauri ya mji wa Geita, Modest Aporinaly alisema shule hizo za msingi na sekondari zinajengwa kwa mapato ya ndani ya halmashauri hiyo .

Alisema fedha za ujenzi wa shule hizo zinatokana na sehemu ya fedha zilizotolewa na Mgodi wa Geita (GGM) kama sehemu ya kurejesha sehemu ya mapato yake kwa jamii (CSR) kiasi cha Sh4.9 bilioni na makusanyo mengine.

"Kufikia mwakani shule zitaanza kupokea wanafunzi na tuna uhakika hakuna mtoto ambaye anakosa nafasi ya masomo," alisema

Akizungumzia miradi hiyo, mchumi wa halmashauri ya mji wa Geita, Emmanuel Malima alisema wanatarajia kujenga Shule ya Sekondari Lukaranga ambayo itagharimu Sh234 milioni na Shule ya Msingi Magogo itakayogharimu Sh234 milioni.

"Pia fedha hizi za CSR tunatarajia pia zitumike kujenga vituo vya afya na zahanati 14 zimejengwa na sasa ujenzi wa misingi ya majengo 22 unaendelea katika hatua mbalimbali," alisema.

Naye ofisa elimu taaluma wa halmashauri ya Geita, Mary Venance alisema ujenzi wa shule za msingi na sekondari katika halmashauri hiyo utaondoa upungufu wa vyumba vya madarasa katika wilaya hiyo.

"Majengo yote yanakwenda vizuri na tuna imani hakuna mtoto ambaye atafikia umri wa kwenda shule na kukosa madarasa na wale ambao watafaulu kidato cha kwanza wote watapata madarasa," alisema.

Halmashauri ya mji wa Geita hadi sasa ina jumla ua shule 61 za msingi na 10 za sekondari.