Mkuchika awaonya ma-DC, RC kuwaweka watu ndani

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora), George Mkuchika

Muktasari:

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Utumishi wa Umma na Utawala Bora), George Mkuchika amesema sheria inayompa mamlaka mkuu wa wilaya kumweka mtu ndani kwa saa 24 inahusu usalama wa mhusika tu na si vinginevyo.

Dodoma. Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora), George Mkuchika amewaonya viongozi, wakiwamo wakuu wa Wilaya na Mikoa akiwataka kutumia madaraka yao vizuri, kuacha kuwaweka watu ndani.

Mkuchika ametoa kauli hiyo leo Jumatatu Desemba 3,  2018 katika ufunguzi wa mafunzo ya wakuu wa mikoa na makatibu tawala wa mikoa yaliyoandaliwa

na taasisi ya Uongozi.

“Mimi sina mipaka naangalia utawala kokote pale, wewe DC (mkuu wa wilaya) madaraka yako ni kumweka ndani mtu saa 24,  umemweka saa 48 nampigia simu bosi wako kwa sababu umetumia madaraka vibaya,” amesema Mkuchika.

Amesema mtu aliyewekwa ndani kwa muda huo (saa 24) kinyume cha sheria akienda mahakamani mhusika atashtakiwa kwa kuvunja sheria.

Mkuchika amesema baada ya mafunzo yaliyotolewa na taasisi ya uongozi, hekaheka za wakuu wa wilaya kuwaweka ndani watu zitapungua.

“Mimi nilikuwa DC miaka 14, nilikuwa RC miaka minane sikumweka mtu ndani hata siku moja. Sheria inasema unamweka mtu ndani kwa usalama wake au ameua na ndugu wa marehemu wanataka kulipiza kisasi hapo unaenda unamficha ndani,” amesema Mkuchika huku akishangazwa na viongozi hao kuwaweka ndani watu waliochelewa kwenye mkutano.

Amesema sheria za utumishi wa umma zina kifungu cha kushughulika na mtu aliyechelewa katika mikutano, na kwamba kumuweka ndani mtu aliyechelewa  mkutanoni ni uvunjifu wa sheria.

Amewataka wakuu hao wa mikoa kuendesha Serikali kwa mujibu wa sheria, taratibu na kanuni na kwamba akisikia jambo haliendi sawa anampigia simu mhusika.

Katibu Mkuu Ofisi ya Rais (Tamisemi), Mussa Iyombe amesema kuna tatizo la kutoelewana kati ya viongozi na kwamba linatokana na kutofahamu mipaka ya kazi zao.