Jafo, Mkuchika wajifungia saa 10 kutatua mgogoro RC, ma-DC

Muktasari:

  • Mawaziri wa Tamisemi, Selemani Jafo na Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Mkuchika wamebisha hodi mkoani Kilimanjaro kutafuta suluhu tatizo la uhusiano uliolegalega kati ya mkuu wa mkoa huo, Anna Mghwira na baadhi ya wakuu wa wilaya.

Moshi. Mawaziri wawili wamebisha hodi mkoani Kilimanjaro kutafuta suluhu ya uhusiano baina ya wateule wa Rais unaolezwa kulegelega.

Mawaziri hao; wa Tamisemi, Selemani Jafo na Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Mkuchika ujio wao ni agizo la Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Desemba 3, 2018 akiwa jijini Dodoma, Majaliwa aliwaagiza mawaziri hao kwenda Kilimanjaro kutatua tatizo la uhusiano uliolegalega kati ya mkuu wa mkoa huo, Anna Mghwira na baadhi ya wakuu wa wilaya.

“Kilimanjaro bado kuna shida. Kuna shida ya mahusiano kati ya mkuu wa mkoa na wakuu wa wilaya, tena wengi siyo mmoja,” alisema Waziri mkuu na kuwaagiza Jafo na Mkuchika kutatua.

Alikwenda mbali na kumuagiza Mkuchika kwenda kuendesha semina ya wakuu wa wilaya juu ya itifaki na kuheshimu mamlaka ya watu wengine ili kuwezesha kazi zifanyike vizuri.

Lakini kabla ya tamko hilo lilitanguliwa na lile la Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan akiwa wilayani Rombo ambaye alikemea uwepo wa uhusiano mbaya wa watendaji wa Serikali.

Ingawa Samia hakueleza wazi, lakini taarifa zinaeleza upo uhusiano usioridhisha kati ya mkuu wa mkoa na wakuu wa wilaya; wakuu wa wilaya na makatibu tawala na wakuu wa wilaya na wakurugenzi.

Mawaziri walivyojifungia saa 10

Jafo na Majaliwa juzi walijifungia katika kikao cha faragha kwenye ukumbi wa mkuu wa mkoa mjini hapa kwa saa 10 kuanzia saa 3:00 asubuhi hadi saa 12.05 jioni.

Mwananchi lililopiga kambi eneo hilo liliwashuhudia wakizungumza na wateule hao wa rais kwa muda, huku kabla ya kikao cha wote aliitwa mtendaji mmoja baada ya mwingine kuingia.

Viongozi waliokutana na mawaziri hao ni mkuu wa mkoa, katibu tawala wa mkoa, wakuu wa wilaya, makatibu tawala wa wilaya na wakurugenzi wa halmashauri za wilaya na manispaa.

Hata hivyo, baada ya kumalizika kwa kikao hicho kilichoendeshwa kwa usiri mkubwa, Mkuchika hakuwa tayari kuzungumza kwa madai kuwa kilikuwa cha ndani na si jambo la kuzungumzia. “Mnihoji mambo mengine, kama ni ya Tamisemi mhojini waziri (Jafo). Ya Utumishi mnihoji mimi, lakini kuhusiana na kikao cha leo kilikuwa cha ndani na hakuna mazungumzo kabisa,” alisema Mkuchika.

Hata hivyo, Jafo kwa upande wake alisema walifika Kilimanjaro kufanya kazi maalumu ya uhusiano kama walivyoagizwa na Waziri Mkuu na kwamba hawawezi kueleza kazi hiyo wameifanya vipi.

“Tumefanya kazi maalumu ya kimahusiano. Sitaki kusema kazi hiyo tumeifanya vipi, lakini imani yangu ni kwamba baada ya kikao chetu kirefu cha leo kila kitu kitaenda vizuri,” alisema Jafo.

Alisema, “Tumekuja kwa ajili ya mahusiano maana haya ni maelekezo kwamba Mkoa wa Kilimanjaro ulikuwa haufanyi vizuri, kwani tulipokuja hapa na Makamu wa Rais alizungumza wazi Kilimanjaro una shida”.

Waziri Jafo alisema wakati Waziri Mkuu akifungua mafunzo ya wakuu wa mikoa na makatibu tawala wa mikoa mjini Dodoma alieleza kuwa Kilimanjaro kuna matatizo ya uhusiano baina ya viongozi na kuwatuma wao kutatua.