Bongo aenda Morocco leo kwa matibabu

Muktasari:

  • “Kesho Jumatano (leo) Novemba 28, Ali Bongo Ondimba, mume wangu, atatoka katika Hospitali ya Mfalme Faisal ya jijini Riyadh, Saudi Arabia,” aliandika Sylvia, mke wa Bongo.

Libreville, Gabon. Rais Ali Bongo Ondimba, ambaye alilazwa katika Hospitali ya Mfalme Faisal jijini Riyadh, Saudi Arabia tangu Oktoba 24, ataruhusiwa kutoka Jumatano na atakwenda Rabat, Morocco kwa matibabu ya kumrejeshea uwezo wake.
Taarifa juu ya Bongo kuondoka Riyadh ilitolewa Jumanne na mkewe, Sylvia, kupitia ukurasa wake wa Facebook.
“Kesho Jumatano (leo) Novemba 28 (…), Ali Bongo Ondimba, mume wangu, atatoka katika Hospitali ya Mfalme Faisal ya jijini Riyadh, Saudi Arabia,” aliandika Sylvia, na akaongeza kuwa atawasili siku hiyo hiyo “Rabat”.
Mwanamama huyo amesisitiza kwamba yeye na mumewe “wanapenda kutoa shukrani zao za dhati kwa mamlaka za Saudi Arabia na timu ya madaktari.”
"Ili kuendelea kupata matibabu hadi apate nafuu, Rais, kwa ushauri wa ndugu wa karibu wa familia yake, waliamua kukubali ombi kutoka kwa kaka yake Mheshimiwa Mfalme wa Morocco Mohammed VI. Tunamshukuru kwa dhati," alisema Sylvia Bongo.
Alisema kuhamishwa kwake kutoka Riyadh hadi Rabat “kumewezekana shukrani kwa nafuu kubwa aliyopata” mumewe.
Rais Bongo anafikiria "kunufaika na kipindi kifupi cha tiba hadi apone hadi mwili kuwa na uwezo kabisa, pamoja na kutekeleza majukumu yake kwa kupitia mafaili muhimu” ya Gabon, alisema mkewe.