Kamati ya Tanzanite yaingia kazini

Rais John Magufuli
Muktasari:
Mwenyekiti wa kamati hiyo Waziri wa Katiba na Sheria Profesa Palamagamba Kabudi
Dar es Salaam. Kamati iliyoundwa na Rais John Magufuli kuchunguza biashara ya madini ya Tanzanite imeanza kufanya mazungumzo na kampuni ya Tanzanite One.
Mwenyekiti wa kamati hiyo Waziri wa Katiba na Sheria Profesa Palamagamba Kabudi amesema mazungumzo hayo yaliyoanza jana Januari 16 , 2018 yanalenga kuhakikisha Tanzania inanufaika ipasavyo na rasilimali ya madini hayo ambayo yanachimbwa nchini Tanzania pekee.
Profesa Kabudi amesema mazungumzo yameanza vizuri ambapo pande hizo mbili zinapitia matatizo yote yanayohusu biashara ya madini ya Tanzanite, utekelezaji wa sheria na kanuni mbalimbali za madini na mapato ya rasilimali hiyo, ili hatimaye zikubaliane namna bora itakayohakikisha Tanzania inanufaika ipasavyo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Tanzanite One B. Faisal Juma Shahbhai amesema Tanzanite One ipo tayari kwa majadiliano hayo na inaunga mkono juhudi za kuhakikisha madini hayo yanainufaisha Tanzania tofauti na ilivyo sasa ambapo yanazinufaisha zaidi nchi nyingine ambazo hazizalishi Tanzanite.
Shahbhai ameongeza kuwa Tanzanite One itatoa taarifa zote zinazohitajika na wakati wote itatoa ushirikiano wenye lengo la kufanikisha mazungumzo hayo.