Kalanga atetea ubunge wake Monduli

Mbunge wa Mteule wa jimbo la Monduli, Julius Kalanga akionesha cheti baada ya kutangazwa mshindi wa uchaguzi mdogo uliofanyika jumapili. Picha na Filbert Rweyemamu

Monduli. Mgombea ubunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Julius Kalanga ametangazwa kuwa mshindi wa uchaguzi mdogo baada ya kupata kura 65,714 sawa na asilimia 95 ya kura zote.

Akitangaza matokeo hayo majira ya saa sita usiku Msimamizi wa uchaguzi katika jimbo hilo, Stephen Ulaya alisema shughuli za uchaguzi huo zilienda vizuri hadi hatua kutangazwa.

Alisema wagombea vyama nane walichuana kuwania jimbo hilo ambalo liliachwa wazi na aliyekua mbunge wa jimbo hilo kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Julius Kalanga aliyejiunga CCM.

Wagombea wengine ni Yonas Laizer wa Chadema aliyepata kura 3,187 ,Wilfred Mlay wa ACT Wazalendo kura 144,Feruz Juma wa NRA alipata kura 45,Simon Ngilisho wa Demokrasia Makini kura 35.

Wagombea wengine ni Omary Juma wa DP aliyepata kura 34,mgombea wa ADA-Tadea,Francis Ringo kura 21 huku Elizabeth Salewa wa chama cha Wakulima alipata kura 16.

Baada ya kutangazwa matokeo hayo na kukabidhiwa cheti,Kalanga aliwashukuru waliomchagua na kuahidi atawatumia kwa nguvu zote.

Alitaja vipaumbele vyake kuwa vitakua kuhakikisha wananchi wanapata maji kwaajili ya matumizi ya binadamu na mifugo pia utatuzi wa migogoro ya ardhi inayokwamisha shuguli za maendeleo.

"Hizi ndizo ajenda zangu muhimu nitakazozisimamia kikamilifu nikishirikiana na viongozi wenzangu kuhakikisha Monduli inabadilika,"alisema Kalanga

Naye Naibu Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia ambaye ni Mbunge wa Ngorongoro,William Ole Nasha alisema CCM imepata ushindi kutokana na kampeni za kiistarabu ilizofanya sanjari na kueleza mafanikio yaliyofikiwa katika kipindi kifupi cha uongozi wa Rais John Magufuli.

"Wananchi wametuelewa na hii ni salamu kwenye majimbo mengine yanayoongozwa na upinzani mkoa wa Arusha na nchini kwa ujumla kuwa siasa za ugomvi hazina nafasi bali wananchi wanataka maendeleo,"alisema Ole Nasha

Baadhi ya wabunge waliokuwepo wakati matokeo yakitangazwa ni mbunge wa jimbo la Longido, Steven Kiruswa, mbunge wa Siha, Dk Godwin Mollel, wabunge wa viti maalum Martha Mlata na Catherine Magige na viongozi wa CCM .