Jafo atoa neno kufutwa matokeo darasa la saba

Muktasari:

  • Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) leo Oktoba 2, 2018 limetangaza kufuta matokeo ya mtihani wa darasa la saba kwa baadhi ya shule za msingi za mikoa ya Dodoma, Dar es Salaam na Mwanza baada ya kubainika kufanya udanganyifu

Dodoma. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo amesema watu wote waliohusika katika udanganyifu wa mitihani ya darasa la saba watachukuliwa hatua.

Shule zilizofutiwa mitihani ya Taifa ya darasa la saba ni shule zote za msingi za Halmashauri ya Chemba mkoani Dodoma, shule Kondoa Integrity iliyopo mji wa Kondoa mkoani Dodoma; Hazina, New Hazina,  Aniny Nndumi na Fountain Of Joy (Dar es Salaam), Allince, New Alliance na Kisiwani zote za Mwanza.

Akizungumza leo Oktoba 2, 2018 baada Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) kutoa taarifa ya udanganyifu wa mitihani ya darasa la saba Jafo amesema si jambo jema lililotokea na kuwasihi Watanzania kuacha tabia hiyo.

“Watu wote waliohusika na ubadhilifu huo watachukuliwa hatua kwa maana jambo hilo halina mjadala na ndio maana wizara yetu kwa kushirikiana na wizara ya elimu iliamua kufanya uchunguzi kubaini waliohusika katika eneo hilo. Watu wote waliohusika watachukuliwa hatua za kiserikali,” amesema.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Binilith Mahenge amesema wameutia Mkoa wa Dodoma aibu ya kufutiwa matokeo ya shule zote za msingi wilaya ya Chemba na Shule moja ya Wilaya ya Kondoa kwa sababu ya baadhi ya watu kushindwa kuzingatia maadili.

“Uingereza ina center nyingi sana za kufanya mitihani duniani ya Cambrige umewahi kusikia kuwa imevuja? Maana yake wenzetu wakila kiapo wamekula kiapo. Hata kama ingekuwa ni mwalimu hawezi kumuibia mtihani mwanafunzi lakini sisi changamoto yetu ni mwalimu anageuka anakuwa lugha moja na mwanafunzi,” amesema.

Amewataka Watanzania kujifunza kwa Uingereza ambao wanatunga mitihani ya dunia nzima lakini imekuwa haivuji.

“Tumefika hapa kwa sababu ya watu kutozingatia maadili na watu kutozingatia kiapo walichokula katika suala la mitihani sasa  hiyo ndio inawaponza watoto hawa. Sasa wajiandae kufanya tena mitihani ya Taifa,” amesema.