JPM mbioni kuhamia Dodoma

Rais John Magufuli

Muktasari:

  • Rais Magufuli amesema pamoja na majengo ya Ikulu Serikali itajenga miundombinu mingine zikiwemo reli na barabara za lami zitakazounganisha maeneo ya vijiji vinavyozunguka Ikulu na mji wa Serikali.
  • Amewahakikishia wananchi kuwa wote watakaoguswa na shughuli za ujenzi wa miundombinu ya Serikali na wanaostahili kulipwa fidia watalipwa, na ametoa wito kwa wananchi hao kutumia fedha za fidia watakazolipwa kujenga makazi bora na kujipanga kufanya shughuli zenye manufaa kwao.

Dar es Salaam. Rais John Magufuli leo (Alhamisi) ametembelea eneo la ujenzi wa Ikulu Chamwino, Mkoani Dodoma na kuwahakikishia wananchi kuwa atahamia Dodoma hivi karibuni kama alivyoahidi.

Rais Magufuli amesema pamoja na majengo ya Ikulu Serikali itajenga miundombinu mingine zikiwemo reli na barabara za lami zitakazounganisha maeneo ya vijiji vinavyozunguka Ikulu na mji wa Serikali.

Amewahakikishia wananchi kuwa wote watakaoguswa na shughuli za ujenzi wa miundombinu ya Serikali na wanaostahili kulipwa fidia watalipwa, na ametoa wito kwa wananchi hao kutumia fedha za fidia watakazolipwa kujenga makazi bora na kujipanga kufanya shughuli zenye manufaa kwao.

“Hapa sasa watakuja watu wengi, wafanyakazi na wageni maana tayari mabalozi wa nchi mbalimbali nao watajenga ofisi zao hapa, sasa na nyinyi mjipange kufanya biashara, mtapata soko la kuuza mazao na bidhaa nyingine, mkipata fedha ziwasaidie kwa manufaa na sio kuzichezea,” amesema Rais Magufuli.