Hatima ya Lissu imo mikononi mwa DPP - Mbowe

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe

Muktasari:

Lissu, ambaye ni mwanasheria mkuu wa chama hicho kikuu cha upinzani, anashikiliwa na polisi tangu juzi jioni alipokamatwa kwenye viwanja vya Bunge mjini Dodoma kwa madai ambayo Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Siro alisema ni kutokana na matamshi yake.

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema hatima ya dhamana ya Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu anayeshikiliwa na polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam imo mikononi mwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) atakayepelekewa jalada lake.

Lissu, ambaye ni mwanasheria mkuu wa chama hicho kikuu cha upinzani, anashikiliwa na polisi tangu juzi jioni alipokamatwa kwenye viwanja vya Bunge mjini Dodoma kwa madai ambayo Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Siro alisema ni kutokana na matamshi yake.

Mbunge huyo aliyefikishwa Dar es Salaam usiku, jana alianza kuhojiwa kwa madai ya uchochezi.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutoka kumwona Lissu katika kituo kikuu cha polisi Dar es Salaam, Mbowe alisema mbunge huyo alihojiwa kwa saa kadhaa na walipokwenda kwa mkuu wa upelelezi wa kanda hiyo kuulizia uwezekano wa dhamana, waliambiwa hatapewa hadi jalada lake litakapopelekwa kwa DPP ambaye atatoa uamuzi.

Mbowe alisema  Lissu ni miongoni mwa viongozi wa  vyama vya siasa na wa kidini ambao walizungumzia na kutahadharisha hali ya kuwapo kwa njaa, lakini Serikali ilikanusha.