Dreamliner ya ATCL kutua Mumbai Novemba

Muktasari:

Abiria watakuwa wakisafiri moja kwa moja kutoka Dar hadi India bila kuunganisha ndege. Safari hiyo kutumia saa sita


Dar es Salaam. Shirika la Ndege la Air Tanzania (ATCL) linatarajia kuanza safari yake ya Mumbai, India siku yoyote ya mwezi Novemba.

ATCL ambayo itakuwa ikifanya safari tatu kwa wiki (Jumatano, Ijumaa na Jumapili) itatumia ndege yake mpya aina ya Boeing 787-8 (Dreamliner). Muda wa safari unatarajiwa kuwa saa sita.

Bei iliyotangazwa na ATCL kwa safari za Mumbai ni Dola za Kimarekani 286 (Sh653,166) kwa safari moja na Dola za Kimarekani 455 (Sh1 milioni) kwa safari ya kwenda na kurudi.

Mkurugenzi Mkuu wa ATCL, Ladislaus Matindi akizungumza na Mwananchi leo Jumanne, Septemba 25 amesema sasa abiria wa wanaofanya safari kati ya India na Tanzania watapata ndege ya moja kwa moja kwani zilizokuwepo zilikuwa ni za kuunganisha.

 

“Sisi tutakwenda kwa masaa sita mpaka Mumbai, tutakuwa tunaenda ‘direct’ (moja kwa moja) ndiyo maana tutafika haraka, mara ya mwisho Air India ndiyo iliyokuwa inafanya hivyo nayo siku hizi haiji. Safari ya kwanza inatarajiwa Novemba,”amesema Matindi bila kutaja tarehe.

Kuanza kwa safari hiyo kunatazamiwa kuongeza watalii kutoka nchini India kwani wataweza kufurahia kukaa muda mrefu hapa nchini kwakuwa muda wa safari umepunguzwa.

Hivi sasa ATCL ina ndege nne, tatu zikiwa ni aina ya Bomberdier Q400 na moja aina ya Boeing 787-8 Dreamliner, Ndege mpya mbili aina ya Airbus A220-300 zinatarajiwa kuwasili kabla ya kuisha kwa mwaka huu na Dreamliner nyingine mwaka 2019.