Dk Kigwangalla kutoa kauli kuhusu ujangili

KOVA KUONGOZA KAMATI YA KUCHUNGUZA WATUHUMIWA UJANGILI

Muktasari:

Dk Kiwangalla asema mshahara wa dhambi ni mauti.

Dar es Salaam. Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla anatarajiwa kutaja hadharani majina ya watu wanaotuhumiwa kwa ujangili nchini.

Kupitia akaunti yake ya Twitter, Dk Kigwangalla amesema atazungumza na waandishi wa habari leo Alhamisi Januari 25,2018 mjini Dodoma kuelezea mambo yanayohusu wizara hiyo.

“Pia nitaweka hadharani watu mbalimbali wanaotuhumiwa kwa ujangili nchini,” ameandika Dk Kigwangalla.

Amesema tangu alipoteuliwa na Rais John Magufuli Oktoba 7,2017 kushika wadhifa huo, alijua kuna mambo mawili ambayo ni changamoto katika wizara hiyo.

 “Nilipoteuliwa nilijua kuna mawili, kujiunga na mtandao wa uovu ili nifaidike binafsi au kuukataa mtandao huu; nilijua kabisa mshahara wa dhambi ni mauti, na kwamba dhuluma haijawahi shinda vita dhidi ya haki, na wala uongo haujawahi shinda vita dhidi ya ukweli,” ameandika Dk Kigwangalla.