Mfanyabiashara ahukumiwa kifungo cha maisha jela

Muktasari:

Rukia ambaye ni mfanyabiashara wa nguo mkazi wa Kinondoni, Dar es Salaam amehukumiwa leo katika Mahakama Kuu Kanda ya Moshi


Moshi. Mfanyabiashara wa nguo mkazi wa Kinondoni Jijini Dar es Salaam, Rukia Mohamed (33) amehukumiwa kifungo cha maisha jela, baada ya kupatikana na hatia ya kusafirisha dawa za kulevya.

Rukia alikamatwa na polisi Desemba 21, 2013 katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kilimanjaro (Kia), akisafirisha gramu 1,471.15 za dawa ya kulevya aina ya Heroin kwenda, Enugu, Nigeria.

Hukumu hiyo imetolewa leo Jumanne Aprili 10, 2018 na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Moshi, Aishiel Sumari ambaye alitupilia mbali utetezi wa mshtakiwa aliyelikana begi lililokuwa na dawa hizo.

Jaji Sumari amesema ushahidi uliotolewa na mashahidi saba wa Jamhuri walioongozwa na wakili wa Serikali mwandamizi, Hassan Nkya na wakili wa Serikali, Ignas Mwinuka ulikuwa ushahidi mzito.

Ushahidi huo ulihusisha ushahidi wa maofisa wakamataji, watunzaji wa vielelezo, mkemia mkuu wa Serikali na vielelezo 11 vinavyohusisha dawa zenyewe, taarifa za kitaalamu na nyaraka za kusafiria.

Jaji Sumari amesema ingawa mshitakiwa alilikana begi lake katika utetezi wake, ushahidi huo hauna msingi kwa vile nyaraka zake za kusafiria zilishabihiana na zilizobandikwa (tag) kwenye begi hilo.

Kwa mujibu wa Jaji Sumari kutokana na ushahidi huo ambao haukuacha shaka mahakama imuona ana hatia ya kosa hilo na adhabu ya kosa hilo ni moja nayo ni kifungo cha maisha jela.

Kufungwa kwa mfanyabiashara huyo kunafanya idadi ya ‘wauza unga’ ambao wamefungwa vifungo cha maisha mkoani Kilimanjaro kwa kusafirisha dawa za kulevya kufikia 11 ndani ya miaka miwili.