Bakhresa kuingia kanda ya ziwa

File Photo

Muktasari:

Mwenyekiti wa kampuni hiyo,  Said Salim Bakhresa amesema ina mpango wa kujenga kiwanda kimoja mikoa ya Kanda ya Ziwa.

Dar es Salaam.  Kampuni ya Bakhresa Group imeeleza azma ya kuongeza viwanda vingine vya usindikaji matunda nchini ili kuongeza thamani kwa mazao ya wakulima.

Mwenyekiti wa kampuni hiyo,  Said Salim Bakhresa amesema ina mpango wa kujenga kiwanda kimoja mikoa ya Kanda ya Ziwa.

Amesema wamefikia uamuzi huo baada ya kubaini kuwa watu wanapata usumbufu wa kusafirisha matunda hadi Dar es Salaam kwa ajili ya soko.

“Kuanzia Oktoba 15, tutaanza kupokea matunda kutoka Kahama na maeneo ya jirani, kwa siku tunapata zaidi ya semi trela 30. Yakimalizika ya kule, tunaanza kupokea mengine kutoka mikoa ya Pwani na Kusini,” amesema Bakhresa.

Amesema “Tukijenga kiwanda Kanda ya Ziwa, tutapunguza kero ya wadau kusafirisha matunda kutoka kule hadi hapa, badala yake tutakuwa tunasafirisha concentrated juice (juisi ghafi) na kuileta hapa kwa hatua zaidi za usindikaji.”

Amesema kampuni hiyo imeajiri zaidi ya wafanyakazi 8,000; wakiwamo Watanzania 180  waliopo kwenye matawi yake nje ya nchi.