Askofu aandika waraka mzito kwa Lissu

Muktasari:

  • Katika waraka huo Askofu Munga ameandika: “Mwanangu TUNDU LISSU:
  • Mungu akupe kupona haraka rafiki na mwanangu wa kiroho. Nilikufahamu muda mrefu na tulipambana pamoja katika ufisadi wa madini kabla hujawa Mbunge.

Dar es Salaam. Askofu Dk Stephen Munga wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini Mashariki ameandika waraka mzito kwa Mbunge wa Singida Mashariki(Chadema), Tundu Lissu akimweleza asiogope.

Katika waraka huo Askofu Munga ameandika: “Mwanangu TUNDU LISSU:

Mungu akupe kupona haraka rafiki na mwanangu wa kiroho. Nilikufahamu muda mrefu na tulipambana pamoja katika ufisadi wa madini kabla hujawa Mbunge.

Ninajua roho yako ya mpambanaji jasiri, shupavu na mwaminifu. Umekuwa sauti ya wanyonge kwa muda mrefu.

Nimeendelea kukufuatilia hata ukiwa bungeni na kuona ni yuleyule ambaye hawezi kunyamazishwa na vitisho vyovyote.

Umeteseka na kuteswa kwa ajili ya kupigania haki za wanyonge. Nilikupigia simu mara kadhaa siku moja kabla ya hiyo siku kushambuliwa kwako lakini sikuweza kukufikia.

Nilichotaka kukuambia ni maneno yaleyale ya siku zote: kwamba usiogope Lissu! Tunaishi kama zawadi ili tupiganie haki za wanaoonewa. Nilipigwa na butwaa kwa habari za kushambuliwa kwako.

Ngoja damu yako iwe mikononi mwao waliofanya hivyo. Wewe utabaki kuwa shujaa katika kumbukumbu za nchi hii.

Ipo siku tutaushinda uovu na haki itatawala. Hakuna mamlaka inayoshinda nguvu na sauti ya wapigania haki. Yeyote aliyefanya hili amefanya kosa kubwa na la kiufundi. Kama utaishi au kama utakufa ujue kwamba wewe ni shujaa.

Lakini nakuhakikishia jambo moja: hatutanyamazia uovu uwao wowote na kamwe hatutaacha kusimama na wale wote wanaotetea kweli na haki.

Hiyo madhabahu iliyoandaliwa kuwachinja watetea haki ipanuliwe maana hiyo iliopo ni ndogo haiwezi kuwabeba wote wenye roho na nia kama yako.

Tunakufa mara moja na baada ya kufa ni uzima wa milele. Kwetu sisi kuishi ni Kristo na kufa ni faida.”