Meli ya matibabu ya Kichina yawa neema kwa wagonjwa Dar

Wagonjwa wakiwa ndani ya meli ya China ‘Ark of Peace’ baada ya kufanyiwa upasuaji wa bure jijini Dar es Salaam jana. Picha na Ericky Boniphace

Muktasari:

Baadhi ya wagonjwa hao Musa Muna (63), ambaye alikuwa akipata matibabu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili amesema ameamua kuacha matibabu hayo kwa muda na kuifuata meli hiyo kutokana na kukosa fedha kiasi cha Sh4.5 milioni za kuondoa uvimbe kwenye figo yake.

       Dar es Salaam. Baadhi ya wagonjwa waliolazwa katika hospitali mbalimbali jijini ikiwemo Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), wameacha matibabu na kwenda kutibiwa kwa madaktari bingwa kutoka China wanaotoa huduma katika meli ya ‘Ark of Peace’ iliyopo bandarini Dar es Salaam.

Baadhi ya wagonjwa hao Musa Muna (63), ambaye alikuwa akipata matibabu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili amesema ameamua kuacha matibabu hayo kwa muda na kuifuata meli hiyo kutokana na kukosa fedha kiasi cha Sh4.5 milioni za kuondoa uvimbe kwenye figo yake.

Alisema baada ya matibabu ya awali alilazwa zaidi ya mara tatu lakini maradhi hayo yamemfanya adidimie kiuchumi na kukosa fedha za matibabu.

Muna alisema alipata taarifa za meli hiyo kupitia redio baada ya tangazo lililoelezea kuhusu huduma hiyo ya matibabu ya Kichina jambo lililomfanya kuja jijini Dar es Salaam kwa treni juzi mchana.

“Nimetoka kijiji cha Mgeta wilaya ni Kilombero, kwa zaidi ya miaka minne nilikuwa natibiwa kliniki Muhimbili ambako pia nimeshalazwa mara tatu, zaidi ya Sh2 milioni nimetumia katika matibabu yangu ya awali, lakini ilishindikana na ili kusafishwa na kuondolewa hicho kiuvimbe ni gharama nisiyoimudu,” alisema Mzee Muna.

“Wakati nasubiria namba nikadondoka ghafla, wakanichukua na kunipa huduma ya kwanza, baadaye nikapatiwa nafasi ya kuonana na RMO (Mganga Mkuu wa Mkoa) na kusaidiwa hivyo nimeambiwa nitapata matibabu Jumamosi,” alisema Muna.

Alisema mwaka 2013 aliambiwa kuwa ana uvimbe pembeni mwa figo na kupewa dawa, lakini hakupona mpaka Oktoba mwaka huu Muhimbili walipomtaarifu kuwa uvimbe umezidi kuwa mkubwa hivyo inatakiwa usafishwe ili kupunguza maumivu yanayomfanya ashindwe kufanya kazi.

Neema Molel, mkazi wa Kimara ambaye amefika kupata matibabu katika meli hiyo alisema baada ya matibabu ya muda mrefu ya mgongo aliyokuwa akiyapata katika moja ya hospitali binafsi jijini ameona ni vema kuwaona wataalamu hao ili apate suluhu ya maumivu hayo.

Alisema tangu mwaka 2014 amekuwa akisumbuliwa na maumivu na madaktari wamekuwa wakimweleza kuwa anatakiwa kupunguza kukaa chini kwa muda mrefu.

“Kuna kipindi niliambiwa nina matatizo ya uti wa mgongo na nilipewa masharti kadhaa, nimekunywa dawa nyingi, lakini naona bado maumivu yanaendelea, nimeona ni vema nikawaona madaktari hawa, na tayari nimepewa namba nasubiri kuitwa,” alisema Neema.

Baadhi ya wagonjwa walifurahia huduma ya haraka waliyokuwa wameipata tofauti na hospitali za kawaida.

Mkazi wa Gongo la Mboto, Victoria Aron alisema huduma aliyoipata ni nzuri na ya muda mfupi ikilinganishwa na sehemu nyingine.

Grace Masanja, mkazi wa Temeke ambaye alilazwa ICU jana kwa ajili ya upasuaji wa jicho usiku wa kuamkia leo amesema anashukuru ujio wa meli hiyo kwani ataweza kupata matibabu bila malipo.

“Muda mrefu jicho lilikuwa linanisumbua na tayari nilikuwa nimeandikiwa rufaa ya kwenda Muhimbili, kwa bahati nzuri imekuja huduma hii na nitafanyiwa upasuaji usiku wa leo (kuamkia leo) na madaktari hawa bingwa bila malipo yoyote,” alisema Grace.

Namba zazua tafrani

Licha ya wagonjwa hao, suala la namba jana lilichukua sura mpya baada ya wananchi kufika katika eneo hilo alfajiri na wengine saa nane usiku ili kuwahi namba lakini wakaelezwa kuwa hakukuwa na utaratibu huo. Tofauti na siku ya awali, jana huduma ilikuwa na malalamiko kutoka kwa baadhi ya wananchi kutokana na namba za huduma hiyo kudaiwa zimeisha.

Baadhi ya wananchi ambao waliwasili kwa usafiri wa treni na daladala walishindwa kupata namba katika eneo hilo, baada ya wahusika kudai kuwa namba zimekwisha hivyo wanatakiwa kuondoka na warejee wiki ijayo.

Mmoja wa wananchi waliotoa malalamiko yao, Arnold Kavishe alisema tangu juzi alfajiri alifika katika kituo hicho kujaribu kupata namba kwa ajili ya matibabu ya mama yake anayesumbuliwa na saratani bila mafanikio.

“Tangu jana hakukuwa na utaratibu mzuri, kadi hazikuwa zikigawiwa kwa utaratibu mzuri askari anakuja anawapa watu anaowajua kadi zaidi ya moja, tupo hapa tangu saa 8 usiku, tukaorodhesha majina ajabu asubuhi wanafika wanasema hatukufuata taratibu, zoezi limesitishwa kwani wameshagawa mpaka watakaotibiwa Jumamosi, wananchi wa chini tunafanyaje? alihoji Kavishe.

Akijibu suala hilo, mganga mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Dk Grace Magembe aliwataka wananchi kuwa na subira kwani mpaka sasa tayari namba za matibabu zimetosha hivyo wasubiri mpaka watakapotangaziwa.

“Tumegawa kadi 6,000 na mpaka sasa watu watakaotibiwa ni mpaka Jumamosi, nasisitiza usinunue kadi kwa mtu subiri mpaka upewe,” alisema Dk Magembe.

Maajabu ya ‘Ark of Peace’

Ndani ya meli hiyo kuna mandhari ya kipekee na huduma mbalimbali zinazopatikana ikiwemo wodi za wagonjwa, vyumba vya madaktari, vyumba vya upasuaji, ICU, mashine mbalimbali za matibabu ikiwemo kunyoosha mgongo.

Pia ina vyumba maalumu vyenye mashine mbalimbali na vifaa vya kisasa kwa ajili ya vipimo, huku dawa na matibabu yanayotolewa yakiwa ni ya kiasili zaidi.

Meli hiyo ina vitanda 300, kila chumba kuna wahudumu wa afya wanaoshirikiana na madaktari wa China kwa ajili ukarimani.