MwanzoContactsEmail
Home Habari Habari za Kitaifa Mkulo: Uchumi unazidi kukua
BOOKMARK THIS PAGE
Mkulo: Uchumi unazidi kukua  Send to a friend
Saturday, 29 May 2010 09:22

Exuper Kachenje
SERIKALI imesema kuwa ukuaji wa pato la taifa katika unakadiriwa kuongezeka na kwamba pato halisi litakua kwa asilimia 7 katika mwaka 2010.
 
Akiwasilisha taarifa ya mwelekeo wa uchumi kwa mwaka 2009 na mwelekeo katika kipindi cha kuanzia 2010 hadi 2013 mbele ya Kamati ya Bunge ya Fedha na Uchumi, Waziri wa Fedha na Uchumi Mustafa Mkulo alisema kuna matarajio makubwa uchumi kuendelea kukua.
 
Huku akiwaomba radhi wabunge kwa kuchelewa kuwapa nakala ya taarifa hiyo, Mkulo alisema maelezo hayo yalipitishwa juzi asubuhi na Baraza la Mawaziri.
 
"Naomba radhi waheshimiwa kwa kuchelewa kuwapatia nakala ya taarifa hii kwa kuwa imepitishwa jana asubuhi (juzi) na Baraza la Mawaziri hivyo imechelewa kuchapwa,"  Mkulo alisema.
 
Mkulo alisema kuwa katika mwaka 2011, pato halisi la uchumi litakuwa kwa asilimia 7.1, mwaka 2012 asilimia 7.4 na hadi kufikia mwaka 2013 pato halisi la taifa litafikia asilimia 7.8.
 
“Kama ilivyotarajiwa athari za msukosuko wa uchumi zilikuwa za mpito, hivyo ukuaji wa pato la taifa unakadiriwa kuanza kuongezeka. Pato halisi litakua kwa asilimia 7.0 mwaka 2010, asilimia 7.1 mwaka 2011, asilimia 7.4 mwaka 2012 na kuendelea kuongezeka hadi asilimia 7.8 mwaka 2013,” alisema Mkulo.
 
Alifafanua kuwa malengo hayo yanatarajiwa kufikiwa kwa kutekeleza sera na misingi ya uchumi kwa kuzingatia mambo mbalimbali, ikiwemo mwenendo wa uchumi wa dunia na hitaji la kujenga uwezo kukabiliana na athari za msukosuko wa uchumi wa dunia.
 
Alitaja misingi mingine kuwa ni kuendelea kutengemaza vigezo muhimu vya uchumi jumla na maendeleo ya jamii hasa mfumuko wa bei, kuweka msukumo katika utekelezaji Dira ya Maendeleo ya Taifa, Mkukuta awamu ya pili, Kilimo Kwanza na kuelekeza rasilimali kwenye maeneo chochezi ya uchumi kwa haraka zaidi.
 
Kwa mujibu wa Mkulo katika kipindi hicho miradi inayopewa kipaumbele katika mwongozo huo wa bajeti itakuwa ni pamoja na miundombinu, uendelezaji ardhi na makazi pamoja na vitambulisho vya taifa.
 
Vingine ni nishati, viwanda, sekta ya fedha na pia kutaja uchaguzi mkuu ujao wa Oktoba mwaka huu kuwa ni kipaumbele cha kipekee kwa serikali katika mwaka huu kwa lengo la kuhakikisha unafanyika kama ilivyopangwa.
Waziri huyo alisema katika muda huo kasi ya upandaji wa bei inakisiwa kupungua hadi asilimia 8.0 kufikia mwezi Juni mwaka huu na kupungua zaidi hadi asilimia tano ifikapo Juni 2011.
 
Aidha, alisema katika kipindi hicho mapato ya ndani  ya taifa yatafikia uwiano wa asilimia 17.3 kwa mwaka 2010/11; asilimia 17.4 mwaka 2011/2012 na asilimia 17.6 ifikapo mwaka 2012/2013.
 
Alisema serikali pia inalenga kuwa na akiba ya fedha za kigeni itakayokidhi uagizaji bidhaa kutoka nje na huduma kwa kipindi kisichopungua miezi mitano; kuwa na viwango imara vya ubadilishaji wa fedha; kuboresha mazingira ya uwekezaji na kufanya biashara na kuedeleza kilimo na kupunguza viwango vya riba.
Kuhusu biashara, Mkulo alisema Tanzania imeshuka katika vigezo vya urahisi wa kufanya biashara kutoka nafasi ya 126 kati ya nchi 183 na kuwa ya 131 mwaka 2009.
 
Kuhusu mapato  ya ndani, Waziri Mkulo alisema yaliongezeka kwa asilimia 18.1 kufikia Sh4,293.1 bilioni mwaka 2008/09; kutoka Sh3,634.6 bilioni mwaka 2007/08 na kwamba kiasi hicho ni pungufu ya asilimia 10 kwa mwaka 2008/09.
 
Kwa kipindi cha Julai 2009 hadi Machi 2010, mapato ya ndani yalifikia Sh3,490.3 bilioni ikiwa chini ya asilimia 8.7 ya makisio ya Sh3,924.9 kwa kipindi hicho akieleza kuwa hali hiyo ilitokana na athari za kuyumba kwa uchumi wa dunia.
 
Mkulo alisema kwa kipindi cha Julai 2009 hadi Machi mwaka huu matumizi ya serikali yamefikia Sh6,143.9 bilioni kati ya makisio ya Sh6,718.7 kwa kipindi hicho, ikiwa ni upungufu wa asilimia tisa uliotokana na upungufu wa mapato.
 
Wakichangia maelezo hayo wabunge walitaka serikali ieleze itafanya nini kuwezesha wananchi kumiliki uchumi badala ya kumiliki asilimia 10 pekee kama ilivyo sasa.

Add this page to your favorite Social Bookmarking websites
Reddit! Del.icio.us! Mixx! Free and Open Source Software News Google! Live! Facebook! StumbleUpon! TwitThis Joomla Free PHP
 

Add comment

Tumia jukwaa ili kutoa maoni ambayo yatasaidia kulijenga taifa letu. Kumbuka, maoni yako yatapitiwa kwanza kabla hayajarushwa hewani!!!!!!


Banner
  • Kupiga Kura

  • Jumapili


Ajali ya Meli ZnZ inatufundisha nini?