Mzee Majuto aenda India kwa matibabu

Muktasari:

Wasanii wajitokeza kumuaga

Dar es Salaam. Muigizaji na mchekeshaji wa siku nyingi, Amri Athuman maarufu Mzee Majuto leo Mei 4, 2018 amesafirishwa kwenda nchini India kwa ajili ya matibabu baada ya kuugua kwa takribani miezi mitatu .

 

Majuto ameenda India kutibiwa katika hospitali ya Apollo, katika jiji la New Delhi baada ya kusumbuliwa na nyonga iliyosababisha ashindwe kutembea na kupata maumivu makali.

 

Akizungumza na MCL Digital leo, mtoto wake Hamza  Amri amesema anaishukuru Serikali kwa kufanikisha safari hiyo, sambamba na  wadau mbalimbali waliojitokeza kumsaidia mahitaji mengine.

 

"Tunamshukuru Mungu pamoja na Serikali kwa kuweza kufanikisha huduma zote za kusafirishwa na za matibabu huko India,” amesema.

 

Katika safari hiyo Mzee Majuto ameambatana na mkewe Aisha Yusuf na mtoto wake wa kiume, Hamza huku wasanii mbalimbali wakijitokeza kumsindikiza  akiwamo Duma na Florah Mvungi.