Mazingira ya siasa yatajwa kikwazo cha kufufuliwa Azimio la Arusha

Muktasari:

Fedha siyo msingi wa maendeleo bali kuna mambo mengine ya msingi ambayo

Dar es Salaam. Wadau mbalimbali wa siasa wamesema mazingira ya kisiasa  nchini hayaruhusu kufufuliwa kwa Azimio la Arusha kwa sababu misingi yake haiendani ya misimamo ya Serikali ya Awamu ya Tano.

Wadau hao wameyasema hayo leo Desemba 20  wakati wa mhadhara wa Kavazi la Mwalimu Nyerere kuadhimisha miaka 50 ya Azimio la Arusha ambalo liliuawa mwaka 1991 baada ya kuanzishwa kwa Azimio la Zanzibar.

Katika majadiliano hayo, Mtafiti Mkuu wa Repoa, Profesa Samuel Wangwe ambaye ni mgeni rasmi katika mhadhara huo amesema kuna viashiria mbalimbali ambavyo vinaonyesha kwamba Azimio la Arusha linaweza kuhuishwa na kutumika katika Tanzania ya sasa.

Profesa Wangwe amebainisha mazingira hayo yanayoendana na misingi ya Azimio la Arusha kuwa ni dhana ya kufanya kazi, kupambana na rushwa na uhujumu uchumi, maadili ya viongozi wa umma na chama kuongoza dhana ya kujitegemea.

Amesema fedha siyo msingi wa maendeleo bali kuna mambo mengine ya msingi ambayo yamebainishwa kwenye Azimio la Arusha. Mambo hayo ni kufanya kazi ndani ya nchi ili kujitegemea wenyewe.

"Mtazamo kwamba fedha ndiyo msingi wa maendeleo ndiyo umetufanya kuwa tegemezi; tunategemea misaada na mikopo kutoka nje. Mwalimu Nyerere aliwahi kusema misaada haiiendelezi nchi."

"Masuala ya msingi yaliyopo kwenye Azimio la Arusha bado yapo kwenye mazingira ya sasa. Bado azimio linahitajika," amesema Profesa Wangwe na kuingeza kwamba changamoto ni falsafa gani inayoweza kuzaa yote yanayotakiwa.

Hata hivyo, mawazo yake hayo yamepingwa na wachangia katika mhadhara huo uliohudhuriwa na wanasiasa, wasomi, wanafunzi, wajasiriamali na wananchi wa kawaida.

Mkazi wa Kinondoni, Joseph Msindai amesema hali ya kisiasa ya sasa haiendani na mazingira na misingi iliyowekwa kwenye Azimio la Arusha ambayo inatoa fursa kwa nchi kujitegemea yenyewe na kuweka mkazo kwenye maisha ya watu.

Amesema demokrasia imeporomoka katika utawala huu, jambo linalowafanya wananchi wasishiriki kikamilifu kwenye kutoa mawazo yao na kuchangia katika maendeleo ya nchi yao.

"Azimio liliundwa wakati wa chama kimoja lakini sasa tuna vyama vingi, nadhani tutakuwa tunaendeleza dhana ya chama kimoja. Tunataka vyama vyote vitendewe haki na viwe na hadhi sawa," amesema mwananchi huyo.

Akiwa na mtazamo tofauti na huo, mjasiriamali Nobert Singo ameshauri kwamba ni vema misingi ya Azimio la Arusha ikawekwa kwenye Katiba na hiyo ndiyo iwe hitaji kubwa la sasa ambalo ni rahisi kutekeleza.

"Rais wetu amesema Katiba siyo kipaumbele chake, nadhani tulichukulie suala la Katiba mpya kama ajenda ili misingi yote ya kwenye azimio itekelezwe na sisi wananchi tuwe na nguvu ya kuwawajibisha viongozi wetu," amesema kijana huyo.

Kiongozi wa chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe ambaye chama chake kinaunga mkono kurejea kwa azimio la Arusha amesema makosa yaliyofanyika huko nyuma ni kuruhusu ubepari wa dola kumiliki njia kuu za uchumi badala ya kuwamilikisha wananchi.

Zitto amemkosoa Profesa Wangwe ambaye amesema serikali ya sasa inaondoa "maadili" na kuleta maadili kwamba yenyewe inaondoa maadili na kuleta maadili ambayo yanasimamiwa na watu wawili ambao ni Rais na hazina.

"Ni mapema sana kuhitisha  kwamba serikali ya awamu ya tank inarudi kwenye misingi ya Azimio la Arusha. Awamu hii ya sasa haina ideology, ni mjadala mpana sana," amesema mwanasiasa huyo.

Hata hivyo, Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Profesa Mwesiga Baregu ametaka kuwepo kwa mjadala mpana kuhusu kurudi kwa Azimio la Arusha ili liendane na mazingira halisi yaliyopo sasa.

Profesa Baregu ameibua maswali ya mjadala kwamba Azimio litakalorudishwa liwe na sura gani? Liambatane na masharti yapi? Na masuala gani yaangaliwe kama kipaumbele. Mwanasiasa huyo ameonya kwamba sasa ni mapema kumtathmini Rais Magufuli na Azimio la Arusha