Ripoti ya CAG inavyowavuruga mawaziri, wenyeviti wa kamati

Muktasari:

Tangu siku hiyo hadi sasa mawaziri sita wamejitokeza mbele ya waandishi wa habari na kujibu masuala mbalimbali kuhusu wizara zao kutokana baada ya ripoti kuibua hoja za ukaguzi.

Aprili 11, mwaka huu Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad aliwasilisha bungeni ripoti ya ukaguzi iliyoishia Juni 30, 2017 na kubainisha mambo mbalimbali, likiwemo la matumizi mabaya ya fedha na ubadhilifu.

Tangu siku hiyo hadi sasa mawaziri sita wamejitokeza mbele ya waandishi wa habari na kujibu masuala mbalimbali kuhusu wizara zao kutokana baada ya ripoti kuibua hoja za ukaguzi.

Kitendo cha mawaziri hao kuendelea kujibu taarifa hiyo ya ukaguzi kulitikisa Bunge baada ya wabunge kuhoji kama wapo sahihi huku Naib Spika Dk Tulia Ackson akieleza kuwa wanachokijibu ni maoni yao binafsi.

Wanaopingana na mawaziri hao wanaeleza wazi kuwa hawapaswi kujibu taarifa ya CAG, kwamba wenye jukumu hilo ni makatibu wakuu wa wizara, wakurugenzi na wenyeviti wa bodi.

Ni ukweli usiopingika kuwa kinachofanywa na mawaziri hao ni kinyume na utaratibu kwa kuwa wanajibu ripoti ya ukaguzi ambayo imeshafungwa tangu mwaka 2017.

Kama kuna ubadhirifu ambao umefanyika katika kipindi hicho, yaani 2016/17 kwa vyovyote vile wao hawawezi kuweka mambo sawa sasa kwa sababu wahusika walioitwa kuhojiwa na CAG walishindwa kutoa ushahidi wa kasoro mbalimbali alizozibaini wakati wa ukaguzi.

Mawaziri waliojibu taarifa ya CAG mpaka sasa ni Dk Charles Tizeba ambaye ni Waziri wa Kilimo, Luhaga Mpina (Waziri wa Mifugo na Uvuvi), Dk Harrison Mwakyembe (Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Charles Mwijage (Waziri wa Viwanda) na Dk Philip Mpango (Waziri wa Fedha) na Seleman Jafo ambaye ni Waziri wa Tamisemi.

Sakata hilo liliibuka juzi baada ya mbunge wa Nyamagana, Stanslaus Mabula kuomba mwongozo akitaka Dk Tulia atoe ufafanuzi kama mawaziri hao wako sahihi kujibu hoja za CAG.

Hoja ya Mabula iliwekewa msisitizo na mbunge wa Ulanga (CCM), Goodluck Mlinga aliyetaka kujua kama kinachojibiwa na mawaziri hao ndio itakuwa mwisho wa kutohojiwa kwa masuala nyeti yaliyoainishwa katika taarifa ya CAG kuhusu wizara zao.

Akizungumzia kitendo hicho, David Silinde (Momba, Chadema) amesema kinachofanywa na mawaziri ni hofu kwa Rais John Magufuli kwa kuwa sekta wanazozisimamia zimetajwa kwa sehemu kubwa hivyo wanaogopa kutumbuliwa.

Silinde ameonyesha kushangazwa na majibu hayo ya wateule wa rais, kubainisha kuwa ukaguzi huo umefanyika kipindi ambacho mawaziri hao walikuwa hawajateuliwa, kama ni kutumbuliwa jambo hilo haliwezi kuwakumba.

“Waache kujitetea wasubiri tukifika kwenye kamati maana wakifanya hivyo sasa mbele ya kamati itakuwaje,” amehoji Silinde.

Naye Ali Hassan Omar (Jang’ombe, CCM) amesema kitendo cha mawaziri kujibu hoja za CAG mbele ya waandishi wa habari ni sahihi kwa maelezo kuwa hata CAG huzungumza ukaguzi wake kwa waandishi wa habari.

Omar amesema hakuna sheria kwa mkaguzi kupeleka taarifa kwa waandishi wa habari kwa madai kuwa kitendo hicho ni kama kuwashtaki waliotajwa kwenye ripoti, kwamba ndio maana mawaziri hao nao wameamua kujibu.

Wakati wabunge wakieleza hayo, juzi Dk Tulia alitoa mwongozo ulioombwa na Mabula na Mlinga, akisema si dhambi mawaziri kujibu hoja, ila wanapaswa kutoa majibu katika kamati za Bunge na kwamba wanachokifanya sasa ni kutoa maoni yao binafsi.

Alisema kwa mujibu wa sheria ya ukaguzi wa umma, mawaziri hao wanapaswa kutoa majibu katika vikao vya Kamati za Bunge.

“Sheria kama ambavyo haimkatazi CAG kuzungumza na vyombo vya habari, kwa namna hiyohiyo haimkatazi mtu yoyote kuzungumzia taarifa ya CAG. Haijasema CAG azungumze na vyombo vya habari na pia haijamkataza mtu yoyote kuzungumzia taarifa hii,” amesema Dk Tulia.

“Ndio maana baadhi ya vyama vya siasa vimeshaeleza kile vinachoona inafaa baada ya kutajwa kwenye ripoti. Sheria hizi mkizipitia waheshimiwa wabunge mtaona. Majibu huwa hayatolewi kwa mdomo. Mawaziri wanatoa mawazo yao.

“Kwa hiyo waziri anavyotoa maelezo si kwamba wamejibu hoja za CAG. Hoja za CAG zinajibiwa kwenye kamati kwa mujibu wa sheria. Anayejibu kwenye kamati ni ofisa masuhuli husika. Msitake kuliweka hili jambo kuonyesha hakuna utawala wa sheria nchini. Sheria zipo na mzisome vizuri kuliko kutoa maelezo ya kuchanganya umma.”

Dk Mwakyembe, ambaye alizungumzia umuhimu wa mawaziri kwenda kwa pamoja mbele ya waandishi kujibu hoja hizo, amesema ukaguzi haumzuii waziri kueleza kilichoainishwa katika ripoti ya ukaguzi.

“Hakuna dhambi kutoa maelezo maana ukaguzi wake ni wa mwaka 2016/17. Hivi tangu wakati huo mpaka sasa ina maana wizara haijafanya chochote kuhusu kilichoelezwa. Tunamuunga mkono CAG na tunampongeza ndio maana kila mwaka tunazidi kufanya vizuri zaidi,” amesema.

Kamati PAC, LAAC wapinga

Utaratibu huo wa mawaziri ni wazi kuwa umewakera wenyeviti wa kamati za Bunge za Hesabu za Serikali (PAC) na Hesabu za Serikali za Mitaa (Laac).

Mwenyekiti wa PAC, Naghenjwa Kaboyoka amesema kinachofanywa na wabunge si sahihi kwa sababu wanaopaswa kujibu taarifa ya CAG ni makatibu wakuu wa wizara pamoja na wenyeviti wa bodi na wakurugenzi wa mashirika na taasisi za Serikali.

“Taarifa ya CAG ina utaratibu wake wa jinsi ya kujadiliwa, ukiona mpaka inaletwa bungeni, maana yake waliopaswa kujibu walikosa majibu maana hupewa siku 21 kutoa ufafanuzi kama wanakuja na taarifa zisizoridhisha,” amesema.

“Kwa sasa CAG ameshaleta taarifa yake kuonyesha jinsi fedha zilivyotumika. Taarifa ikishawasilishwa, kamati zetu zinawaita maofisa masuhuli kuwahoji kuhusu kilichomo katika ripoti ya CAG na huwa tunataka taarifa sahihi kwa sababu kama wangekuwa na taarifa sahihi wakati huo wangeziwasilisha, kama wanazo taarifa basi lazima CAG azihakiki kwanza.”

Amesema mawaziri hao wanazungumza ya kwao na kubainisha kuwa kama kuna eneo CAG kaeleza utata wa fedha halafu mawaziri wakisema fedha hizo zimeanza kulipwa ni wazi kuwa zinazolipwa si sahihi kwa sababu ukaguzi ulishafungwa tangu 2017.

“Jambo kama hili halipaswi kuachwa hivihivi. Lazima iangaliwe fedha imechukuliwaje maana huenda ikawa ni cheni kubwa, lazima tujue ni hatua gani imechukuliwa,” alisema mwenyekiti wa Laac, Vedasto Mwiru.

Hoja za CAG hujibiwa baada ya sisi kuwaita wahusika. Waziri anaposema anajibu hayo maoni ya CAG, nani anahakikisha kuwa anachokijibu ni sahihi,” amehoji.