Ma-DC wadaiwa kuitumia vibaya sheria ya kifungo saa 48

Naibu waziri Ofisi ya Rais, Tamisemi, utumishi na Utawala Bora, Seleman Jaffo.

Muktasari:

  • Kwa mujibu wa Sheria ya Tamisemi ya mwaka 1997, kifungu cha 15 (1) inawapa mamlaka wakuu wa mikoa na wilaya kutoa amri ya mtu kukamatwa na kuwekwa ndani kwa saa 48 pale anapobainika kwamba mhusika ametenda kosa fulani.

Dar es Salaam. Amri ya wakuu wa wilaya kuwaweka ndani, baad-hi ya viongozi wa serikali na wale wa kisiasa imeendelea kujitokeza huku wadau wakikosoa suala hilo na kutaka wakuu hao watumie njia ya kuwaonya na si kuwakamata.

Kwa mujibu wa Sheria ya Tamisemi ya mwaka 1997, kifungu cha 15 (1) inawapa mamlaka wakuu wa mikoa na wilaya kutoa amri ya mtu kukamatwa na kuwekwa ndani kwa saa 48 pale anapobainika kwamba mhusika ametenda kosa fulani.

Miongoni wa viongozi na Seri-kali na kisiasa waliowekwa ndani kwa kutumia sheria hiyo ni pamo-ja na meya wa Ubungo (Chadema), Boniface Jacob ambaye aliwekwa ndani na mkuu wa wilaya hiyo, Kisare Makori mwaka jana.

Novemba 2015, Paul Makonda wakati huo akiwa mkuu wa wilaya ya Kinondoni aliagiza kuwekwa rumande kwa saa sita maofisa ardhi 20 wa manispaa ya Kinon-doni kwa kosa la kuchelewa kuwasili katika ziara ya kutatua migogoro ya ardhi.

Inadaiwa kwamba viongozi hao walikuwa wakifanya ziara ya kuangalia namna ya kutatua migogoro hiyo katika kata ya Wazo na kikao kilitakiwa kuanza saa mbili lakini maofisa hao wali-fika baada ya saa tatu.

Makonda pia akiwa mkuu wa wilaya hiyo aliwahi kuamuru kukamatwa kwa Mbunge wa Ubungo Saed Kubenea baada ya kurushiana maneno kati yao.

Oktoba 13, 2017 kaimu mkurugenzi wa wilaya Sengerema, Oscar Kapinga aliswekwa ndani kwa saa 12 na mkuu wa wilaya hiyo kwa kushindwa kutekeleza agizo la kutafuta fedha na kuwalipa wanaofanyakazi za usafi katika mji huo.

Machi 8 mwaka huu Mbunge wa Hana’ng na waziri katika serikali ya Awamu ya Nne, Dk Mary Nagu alikamatwa kwa amri ya aliyekuwa mkuu wa wilaya hiyo Sarah Msafiri kwa kile alichodai mbunge huyo alikuwa anaichonganisha Serikali na wananchi.

Tukio jingine ni la aliyekuwa mkuu wa wilaya ya Arumeru, Alexander Mnyeti aliyewaweka ndani madiwani wanne wa Chadema kwa madai wamekuwa wakikwamisha kutekeleza kazi zake.

Pia kaimu meneja wa Mamlaka ya Maji Mradi wa Makondeko wilayani Newala, Athuman Semkondo naye aliwekwa ndani kwa saa 48 kwa amri ya mkuu wa wilaya hiyo kwa madai ya kuvikosesha maji vijiji 14 vyenye wakazi 60,000.

Agosti 13 mwaka huu, mkuu wa wilaya ya Ilala, Sophia Mjema naye aliamuru diwani wa Kitunda, Nice Gisunte awekwe ndani baada ya kutofautiana naye katika mkutano akidai alitaka kuvuruga ziara yake.

Hawafurahii kamatakamata

Licha ya sheria hiyo kuwepo, lakini imeonekana kutowaridhisha baadhi ya viongozi wa juu wa Serikali kwa namna inavyotekelezwa.

Hivi karibuni akiwa katika kikao cha kazi cha wakuu wa wilaya 27 walioteuliwa hivi karibuni na Rais John Magufuli, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), Seleman Jafo alikemea tabia ya baadhi ya watendaji hao kutumia vibaya madaraka hayo kuwaweka watu ndani.

Alisema tabia hiyo inasababisha wananchi kuichukia Serikali, hivyo ameagiza wakuu wa wilaya kuitumia sheria hiyo kama ilivyokusudiwa na si kwa kuonea watu.

Onyo hilo la Jafo si la kwanza, kwani alipokuwa naibu wa wizara hiyo aliwahi kukemea vitendo hivyo.

Mbali na Jafo, mtangulizi wake katika wizara hiyo, George Simbachawene aliwahi kuwaonya wakuu wa wilaya na mikoa dhidi ya matumizi mabaya ya madaraka yao kutokana na kukamata watu walio kwenye himaya zao.

Si hao tu bali Waziri wa Afya, Maendeleo Jamii, Jinsia, Watoto na Wazee, Ummy Mwalimu aliwahi kukemea tabia ya wakuu wa wilaya na mikoa kuwasekwa rumande watumishi walioko kwenye maeneo yao ya kazi.

Juzi Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), Seleman Jafo alikemea tabia ya baadhi ya wakuu wa wilaya kutumia madaraka yao vibaya kwa kuwaweka watu ndani.

Mwalimu alitoa kauli hiyo wakati akizindua majengo ya wodi ya wazazi na matibabu ya dharura katika Hospitali ya Wilaya ya Bagamoyo, ambapo aliwataka viongozi hao kuacha tabia ya kuwaweka mahabusu watumishi wa umma kwa makosa ya kitaaluma.

Wakizungumza na gazeti hili jana kwa nyakati tofauti wadau hao walisema kuwaweka amri za kuwaweka ndani watumishi wa umma au viongozi wa kisiasa si njia sahihi bali wafuate utaratibu wa kuwawajabisha.

“Jafo katumia busara ya kiuongozi kuwaonya baadhi ya wakuu wa wilaya wanaofanya vitendo hivi. Hiki ndicho kinachotakiwa, si afya kwa kiongozi wa Serikali upo katika mkutano wa hadhara kutoa amri mtumishi fulani awekwe ndani.

“Unachotakiwa ni kutumia busara ya kumwajibisha kwa mujibu wa taratibu lakini si kumweka ndani. Kama kiongozi wa kisiasa mchukulie kama raia wa kawaida muite ofisini kwako na umuonye yeye ni binadamu atajirekebisha, endapo ana kosa la jinai vyombo vya ulinzi vitafanya kazi yake,” alisema Dk Benson Bana

Dk Bana ambaye pia ni mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), alisema kwamba maelezo yaliyotolewa na Jafo kwenda kwa wakuu wa wilaya yapo sahihi na wahusika wayazingatie.

“Jafo ni jembe kweli kweli ninamuunga mkono kwa hatua hii. Narudia tena si afya kusema kiongozi wa kisiasa au Serikali kumweka ndani,” alisema Dk Bana.

Wakati Dk Bana, akieleza hayo mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria (OUT), Hamad Salim alisema kauli hiyo Jafo haitoshi bali kunahitajika marekebisho ya sheria mbalimbali ikiwamo ya kuwapa mamlaka wakuu wa mikoa na wilaya kuwaweka watu ndani kwa saa 48.

Alisema sheria hiyo na nyingine nyingi zilitungwa muda mrefu wakati wa chama kimoja lakini sasa mambo yamebadilika na ni wakati sasa ibadilishwe ili kuendana na kasi ya maendeleo ya Taifa.

“Sheria hii haitumiki ipasavyo kama ilivyoandikwa. Ninachokiona mkuu wa wilaya akikosana au kupishana na mtendaji au kiongozi wa siasa anaamuru awekwe ndani jambo ambalo si sawa.

“Wakuu wa wilaya hawaiangalii vyema sheria hii bali wanaangalia kipengele cha nina uwezo wa kuweka ndani, ”alisema Hamad.

Mbali na hilo, Hamad alisema anachokiona yeye ni utamaduni uliopo kwa baadhi ya wakuu wa wilaya wanaoteuliwa bila kupewa semina elekezi namna ya utendaji kazi wao unavyotakiwa.

Wakati huohuo, Gisunte ameachiwa kwa dhamana jana baada ya kuwekwa ndani Agosti 13 kwa amri ya Mjema.

Akizungumza jana Gisunte alisema alitoka juzi saa tatu usiku baada ya mkuu wa upelelezi kumwambia anatakiwa atafute mdhamini ili aachiwe kwa dhamana.

“Muda wangu wa saa 48 alizosema Mjema zilitakiwa ziishe leo saa 6 mchana (jana). Lakini jana (juzi) mkuu wa upelelezi aliniambia nitafute mdhamini kwa ajili ya kupewa dhamana na leo niende kuripoti tena polisi,” amesema Gisunte.

Akizungumzia jinsi tukio lilivyokuwa, Gisunte alisema si kweli kwamba alitaka kuvuruga ziara ya Mjema bali yeye alikuwa anatimiza majukumu yake kama diwani wa kata hiyo wakati mkuu wa wilaya huyo alitaka kuingiza siasa katika mkutano huo.

Gisunte alisema wakati Mjema anaHutubia wakazi wa Kitunda alikuwa kimya na mtulivu akimsikiliza lakini aliingiza siasa kwa kutoa salamu za CCM katika mkutano wa Serikali.

Alisema alihoji kwa kumwambia kwamba akitumia salamu za CCM naye akisema za Chadema itakuaje? kwa sababu ndiyo ninayeongoza kata hiyo. Nilimwambia hupaswi kufanya hivyo.

“Baada ya kauli hii, Mjema aliagiza polisi wanikamate na kuniweka ndani. Nilisema baadhi ya viongozi wanatumia madaraka yao vibaya ni vyema wakatenganisha shughuli za chama na Serikali,” amesema Gisunte.