Jaji Mihayo atoa elimu adhabu ya faini na kifungo jela

Jaji mstaafu Thomas Mihayo.

Muktasari:

  • Akizungumza na Mwananchi jana kuhusu namna vyombo vya habari vinavyoripoti adhabu hizo Jaji Mihayo alisema kumekuwa na upotoshaji katika eneo hilo, jambo ambalo linaweza kuleta matatizo kwa chombo cha habari na kwa mtu aliyehukumiwa.

Dar es Salaam. Jaji mstaafu Thomas Mihayo amewashauri waandishi wa habari kuripoti vizuri uamuzi unotolewa na Mahakama nchini hasa kwenye adhabu zinazohusisha faini au kifungo jela.

Akizungumza na Mwananchi jana kuhusu namna vyombo vya habari vinavyoripoti adhabu hizo Jaji Mihayo alisema kumekuwa na upotoshaji katika eneo hilo, jambo ambalo linaweza kuleta matatizo kwa chombo cha habari na kwa mtu aliyehukumiwa.

Alisema mtu anapohukumiwa kulipa faini, Mahakama hutoa mbadala wa adhabu hiyo ambao huwa ni jela, hivyo anapolipa faini anakuwa ameepuka kwenda jela lakini anaposhindwa kulipa anakwenda jela hadi atakapoweza kulipa faini.

“Adhabu ya kwanza ambayo ndiyo ya msingi inakuwa ni faini na isipolipwa linalofuata ni jela, lakini akifanikiwa kuzipata hizo fedha na kulipa baada ya kwenda jela, atatolewa ila kuna hesabu zitafanyika ili kupunguza kiwango cha fedha za faini kutokana na muda ambao mtu huyo ameshatumikia jela,” alisema Jaji Mihayo.

Alisema nje ya utaratibu huo, vyombo vya habari vimekuwa vinavyoripoti kuwa mtu fulani amehukumiwa kwenda jela au kulipa faini, hivyo kuifanya adhabu ya msingi kwa mtu huyo ni kifungo.

Kutokana na upotoshaji huo, Jaji Mihayo alisema mtu huyo akiachiwa huru baada ya kukamilisha faini anaweza akapata matatizo kwa kuwa watu watashangaa wakihoji mbona imeelezwa amekwenda jela halafu yuko nje.

“Inapopotoshwa adhabu aliyopewa mtu unamkosesha mambo mbalimbali na hivyo anaweza kukushtaki kwa upotoshaji huo,” alisema Jaji Mihayo.

Alifafanua kuwa inapotokea adhabu ya kwanza ya msingi kwa mshtakiwa ni jela, kwa kawaida hakuna mbadala wake.

Kujumlisha adhabu

Jaji huyo alisema vilevile, vyombo vya habari vimekuwa vikipotosha kwa kujumlisha adhabu za makosa tofauti pale zinapotekelezwa kwa wakati mmoja. “Unakuta mtu amehukumiwa kwa makosa manane kulipa faini Sh200,000 kila kosa na adhabu zote zinakwenda pamoja, wao wanajumlisha na kuandika kuwa atalipa Sh200,000 mara nane, wakati ukweli ni kwamba mtu huyo atalipa Sh200,000 tu kwa kuwa adhabu zote zinaambatana.

Aliongeza kuwa kwa makosa hayo manane kama adhabu ni miaka mitatu mitafu, kama zinaambatana atafungwa miaka mitatu na si miaka mitatu mara nane kama ambavyo imekuwa ikiripotiwa.