Filamu ya pacha inaendelea

Asma Juma na mumewe Aboubakar Pazi wakiwa na mtoto wao wanayedai alitakiwa kuzaliwa na mwenzake pacha  katika Hospitali ya Rufaa ya Temeke Dar es Salaam mwezi uliopita, lakini madaktari waliwapa mtoto mmoja tu. Picha na Salim Shao

Muktasari:

Wakati Dk Malima akisema suala hilo limeshafikishwa ofisi ya Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Kambi amekana kukabidhiwa ripoti hiyo.

Dar es Salaam. Mganga Mfawidhi wa  Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Temeke, Dk Amaani Malima na Mganga Mkuu wa Serikali, Muhammad Kambi wametofautiana kuhusu sakata la mwanamke anayedai alikuwa na ujauzito wa watoto pacha, lakini amekabidhiwa mtoto mmoja.

Wakati Dk Malima akisema suala hilo limeshafikishwa ofisi ya Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Kambi amekana kukabidhiwa ripoti hiyo.

Pia, Profesa Kambi amekana kupata maelekezo kutoka kwa Naibu Waziri wa Afya, Dk Hamis Kigwangalla ya kuunda kamati maalumu ya kuchunguza tuhuma kuwa Hospitali ya Temeke imemuiba mtoto mmoja kati ya pacha hao.

Mwanamke huyo, Asma Juma (29) anadai kuwa alifanyiwa vipimo vya ultrasound kabla ya kwenda hospitalini hapo na aliambiwa kuwa, alikuwa na ujauzito wa pacha.

Juzi, Dk Malima aliliambia gazeti hili kuwa Mganga Mkuu wa Serikali ameunda kamati maalumu kwa agizo la Dk Kigwangala, baada ya kupata malalamiko hayo na kwamba kamati hiyo ilifanya uchunguzi  kwa muda wa juma moja na imeshakabidhi ripoti kwa Mganga Mkuu wa Serikali, Ijumaa iliyopita.

Hata hivyo, alipoulizwa jana kuhusu taarifa za kukabidhiwa ripoti hiyo, Profesa Kambi alisema hajakabidhiwa wala haijafika ofisini kwake na kwamba kama kuna kamati imefanya uchunguzi, hajui imeundwa na nani.

 “Labda itakuwa bado iko katika taratibu za kiofisi. Kwa hiyo kamati haikuundwa na wizara, au itakuwa imeundwa na Mganga Mkuu wa Wilaya, wa Mkoa au mamlaka nyingine,” alisema Profesa Kambi.