... Lugola azungumzia kutoweka kwa Azory Gwanda, atoa kauli tata

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Kangi Lugola akizungumza wakati wa mkutano na waandishi wa habari jijini, Dar es Salaam jana. Picha na Omar Fungo

Muktasari:

Lugola alitoa kauli hiyo jana, wakati wa mkutano wake na wanahabari uliofanyika ofisi ndogo ya wizara hiyo jijini Dar es Salaam.

Dar es Salaam. Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola amesema wizara hiyo haihusiki na kupotea kwa mwandishi wa habari wa Kampuni ya Mwananchi Communications (MCL), Azory Gwanda.

Lugola alitoa kauli hiyo jana, wakati wa mkutano wake na wanahabari uliofanyika ofisi ndogo ya wizara hiyo jijini Dar es Salaam.

Gwanda alitoweka tangu Novemba 21, 2017 nyumbani kwake Kibiti mkoani Pwani, kilomita 130 Kusini mwa Jiji la Dar es Salaam.

Gwanda ni mmoja wa waaandishi wa kwanza kuripoti kwa kina mfululizo wa mauaji yaliyokuwa yakitekelezwa na watu wasiojulikana katika vijiji mbalimbali katika wilaya hiyo yaliyowalenga polisi na viongozi wa vijiji. Wakati wa kutoweka kwa mumewe, mkewe Anna Pinoni alisema watu wanne wakiwa kwenye gari aina ya Toyota Land Cruiser nyeupe walimchukua Gwanda kutoka katikati ya mji huo, mahali ambapo hupendelea kukaa na kuondoka naye.

Lugola atoa kauli tata

Akitoa maelezo baada ya kuulizwa swali na mwandishi aliyehudhuria mkutano huo aliyehoji juu ya watu kupotea akiwamo Gwanda, Lugola alisema kutoweka kwa mtu kunaambatana na utata.

Swali: Mheshimiwa waziri hivi karibuni kumekuwa na matukio ambayo sisi waandishi wa habari yanatusumbua mojawapo ni kupotea kwa mwanahabari mwenzetu, Gwanda ambaye bado hajaonekana tangu atoweke Novemba, mwaka jana. Nini kinachoendelea, hili unalizungumziaje ili waandishi wa habari tufanye kazi katika mazingira salama bila kubughudhiwa?

Lugola: Zipo hizo habari. Mtu yupo nyumbani kwake halafu ametoweka. Sisi (Wizara ya) Mambo ya Ndani hatuingilii uhuru wa mtu au kutoweka nyumbani kwake. Kila mtu ana uhuru kwa mujibu wa Katiba ya nchi anaweza kutoka sehemu moja kwenda nyingine bila kuvunja sheria. Waziri Lugola alisema kama Gwanda alitoweka akiwa nyumbani, wao hawahusiki bali wanahusika kumtafuta mtu aliyetendewa uhalifu ikiwamo kutekwa akisema katika tukio kama hilo vyombo vya dola humtafuta mtekaji.

“Hawa ambao wanatoweka kwao tu, wanakuwa na sababu nyingi. Kuna wengine maisha yakiwashinda anaamua kwenda kwingine,” alisema.